Wafungwa wengine watoroka jela DR Congo

Kinshasa, DR Congo. Wafungwa wengine wametoroka kutoka gereza ikiwa ni siku mbili baada ya zaidi ya wafungwa 3,000 kutoroka kwenye gereza kuu.

Jumatano iliyopita wafuasi wa, Ne Muanda Nsemi kiongozi wa kikundi kimoja cha Kikristo aliyefungwa, walivamia alfajiri na kufanikiwa kumtorosha. Kiongozi huyo wa kundi la kidini linalofahamika kama Bundu Dia Kongo (BDK) alifanikiwa kutoroka pamoja na wafungwa 50, kutoka gereza lililopo jijini Kinshasa.

Msemaji wa serikali Lambert Mende alithibitisha kuwa kiongozi huyo Ne Muanda Nsemi, alifanikiwa kutoroka baada ya gereza hilo kuvamiwa na wafuasi wake.

Jana, taarifa zilisema wafungwa 60 wanadaiwa kutoroka kutoka jela ya Kasangulu, kilomita 40 kutoka mji mkuu Kinshasa. Gereza hilo linapatikana katika eneo ambalo ni ngome ya madhehebu ya Bundu Dia Kongo.

Kwa sasa, maofisa wa serikali walikuwa bado wanatafakari uwezekano wa kutuma jeshi kulinda magereza.