Wafungwa wenye ujuzi watakiwa kusaidia magereza

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Muktasari:

Alitoa mfano wa Gereza la Geita kwamba linapaswa kuwa na wafungwa 100, lakini hivi sasa linao zaidi ya 500 jambo ambalo ni hatari kwa afya.

Chato. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewaagiza maofisa magereza nchini kutumia wafungwa na mahabusu wenye utaalamu wa masuala ya ujenzi, kujenga mabweni na nyumba za watumishi ili kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani. Mwigulu alitoa agizo hilo juzi baada ya kutembelea Gereza la Wilaya ya Geita na kushuhudia msongamano wa wafungwa, hivyo aliwataka maofisa magereza kutumia fedha wanazopewa za ujenzi kununua vifaa.

Alitoa mfano wa Gereza la Geita kwamba linapaswa kuwa na wafungwa 100, lakini hivi sasa linao zaidi ya 500 jambo ambalo ni hatari kwa afya.

Akizungumza katika Gereza la Chato, Kamishna wa Magereza Tanzania, Casmiri Minja alisema magereza wameshindwa kujenga au kuboresha mabweni ya wafungwa kutokana na Serikali kutotoa fedha kwa miaka minne.

Mkuu wa Gereza Mkoa wa Kagera, Jeremiah Nkondo anayesimamia ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Chato alisema likikamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafungwa 50.