Wafurahia ongezeko la watumishi wa umma

Muktasari:

Wafanyabiashara watakiwa kujiandaa kutosheleza mahitaji ya huduma kwa watumishi zaidi ya 15,000 ifikapo Novemba mwaka huu.

Dodoma. Wafanyabiashara wa masoko yaliyopo katika Manispaa ya Dodoma wamesema kuwa wamejiandaa kukabiliana na ongezeko la watu wanaohamia mkoani humo kutokana na ujio wa makao makuu ya Serikali.

Tangu Rais John Magufuli alipotangaza kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma hivi karibuni, kumekuwa na maandalizi kabambe, huku ongezeko la watu likitarajiwa kuwa kubwa mkoani humo.

Mwenyekiti wa Soko Kuu la Majengo katika Manispaa ya Dodoma, Godson Rugazama alisema wamepewa taarifa na Serikali ya mkoa huo kuwa Novemba mwaka huu jumla ya watumishi 15,000 watakuwa wamehamia Dodoma.

Alisema wafanyabiashara wa masoko yaliyopo mjini hapa wamejiandaa kuhudumia idadi hiyo kubwa ya Watanzania kwa kuwa wote watategemea bidhaa kutoka masoko yao.

“Tulikuwa na kikao na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme ambaye alituambia tujiandae kupokea ugeni mkubwa wa watumishi wapato 15,000 ifikapo Novemba mwaka huu kwa kuhakikisha kuwa masoko yetu yanakidhi mahitaji na kuboresha huduma zetu kwa kufanya kazi kwenye mazingira safi,” alisema Rugazama.

Aliongeza kuwa ujio huo wa wageni katika Mkoa wa Dodoma ni neema kubwa kwa wafanyabiashara kwani kutaongeza mapato yao na kukuza uchumi wa wakazi wa Mkoa wa Dodoma katika kila sekta.

Mwenyekiti wa soko la mboga na matunda la Sabasaba katika Manispaa ya Dodoma, Athumani Makole alisema idadi ya masoko yanayopatikana mjini hapa yanakidhi mahitaji ya mkoa huu kuwa makao makuu ya nchi bila wasiwasi wowote.

Alisema kuongezeka kwa idadi ya watu hakuwezi kuwafanya washindwe kuwahudumia kwa kuwa watu wengi hufanya manunuzi ya mwezi mmoja hivyo siyo kila mara watakuwa wanakwenda sokoni.

“Wangekuwa wanakuja sokoni kwa mkupuo hapo kweli tungeshindwa kuwahudumia lakini wanakuja mmoja mmoja tena kila mtu akiwa na mahitaji yake tofauti na mwenziwe hivyo hatutashindwa kuwahudumia,” alisema Makole.

Mfanyabishara wa Soko Kuu la Majengo Iddi Vumba alisema hali ya biashara kwa sasa ni nzuri tofauti na siku zilizopita kabla ya tangazo la kuhamishia makao makuu mkoani humo.

Alisema wananchi wengi wameamua kutumia fursa hii kuanzisha masoko madogomadogo kwenye maeneo yao hivyo kufanya mzunguko wa biashara katika masoko makubwa kuongezeka.