Wagombea udiwani Chadema waenguliwa kwa kutojua kusoma, kuandika

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Aman Golugwa

Muktasari:

Baadhi hawakurejesha fomu, wengine walishindwa mitihani ya kusoma na kuandika.


Arusha. Wagombea 11wa udiwani wa Chadema, wameenguliwa katika uchaguzi mdogo kwa sababu kadhaa ikiwamo kutokujua kusoma na kuandika.

Miongoni mwa wagombea walioenguliwa wapo watano wa wilaya ya Ngorongoro.

Madiwani 19 wa Chadema walijiuzulu nafasi zao na kujiunga na CCM, huku diwani mmoja wa chama hicho kata ya Baray, Moshi Darabe, akifariki dunia. Darabe alikuwa pia Mwenyekiti wa chama hicho Karatu.

Akizungumza leo Julai 17, Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Aman Golugwa amesema kuenguliwa kwa wagombea wake 11 kumetokana na mizengwe ya uchaguzi na vitisho kwa wagombea.

"Hadi sasa ni kweli tumebaki na wagombea 9 tu kati ya kata 20, maeneo yote tulitaraji kuwa na wagombea lakini, wamejiondoa dakika za mwisho, wengine kung'olewa eti hawajui kusoma na kuandika na wengine vitisho hawajarejesha fomu,"amesema.

Amesema katika jiji la Arusha ambapo kunatarajiwa uchaguzi wa kata nne, pia kuna wagombea wawili wa kata ya Osunyai na Kaloleni wamewekeza mapingamizi na tayari yamejibiwa.

"Huu uchaguzi utakuwa mgumu sana tayari tumelalamika tume ya taifa ya uchaguzi na polisi, kuna sehemu mgombea wetu aliambiwa kuandika jina la zinjanthropus na alipokosea akaondolewa eti hajui kusoma na kuandika, mwingine amenyang'anywa fomu mlangoni "amesema

Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe amesema chama hicho, kimejiandaa kurejesha kata zote na wagombea wa Chadema wengi wamejitoa baada ya kubaini hawatoshi katika nafasi walizoomba na hivyo kuwaachia wa CCM.

"Kuna mapingamizi yamewekwa kihalali na wengine wamejitoa baada ya kubaini hawajui kusoma na kuandika," amesema.

Hata hivyo, wasimamizi wa uchaguzi mkoani Arusha, wote walieleza taratibu zote kufuatwa katika uchaguzi, ikiwamo kuenguliwa wagombea wanaokosa sifa.

Msimamizi uchaguzi wilaya ya Longido ambapo uchaguzi ulipangwa kufanyika katika kata tatu, Jumaa Mhina amesema katika halmashauri yake mgombea mmoja wa Chadema kata ya Alang'atadapash Isaya Laizer hakurejesha fomu.

Mhina amesema katika  kata ya Kamwanga mgombea wa Chadema Sakimba Alais pia aliwekewa pingamizi kwa tuhuma za kutojua kusoma.

Msimamizi jimbo la Ngorongoro, Raphael Siumbu amesema katika kata tano, wagombea wanne wa CCM wamepita bila kupingwa.

Amezitaja kata hizo kuwa ni Soitsambu, Pinyinyi, Ngoile na Ngorongoro ambapo kata moja ya Alaitole ndio kulikuwa na mgombea ambaye pia baadaye alijitoa 

Katika halmashauri ya Monduli, Msimamizi wa uchaguzi, Stevin Ulaya amesema kati ya kata  sita,  mbili wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa.

Ulaya amesema wagombea wa Chadema waliochukua fomu hawakurejesha katika kata za Nararami na Loksale na kata nyingine taratibu za uchaguzi zinaendelea

Katika uchaguzi  huo CCM iliwapitisha kugombea madiwani wote 19 wa Chadema waliojiuzulu na kujiunga na CCM.