Muhimbili yashindwa kuhamishia wagonjwa 50 Mloganzila

MABASI YATUMIKA KUHAMISHA WAGONJWA MUHIMBILI

Muktasari:

Ni kutokana na hali zao za kiafya zilivyo

Dar es Salaam. Zaidi ya wagonjwa 50 leo Jumamosi wamekwama kuhamishwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenda Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila (MAMC) kutokana na hali zao kiafya.

Kuhamishwa kwa wagonjwa hao ilikuwa ni mwendelezo wa uteketezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuwaondoa baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika jengo la Mwaisela wapelekwe Mloganzila ili kupunguza msongamano uliopo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi hospitalini hapo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma MUHAS na Mloganzila, Hellen Mtui amesema wagonjwa hao walitarajiwa kuwasili saa tatu asubuhi.

Amesema sababu ya kusitisha zoezi hilo kwa leo, limechangiwa na wengi wao hali zao kubadilika hivyo Muhimbili wameshindwa kuwasafirisha wachache.

"Wenzetu wametupatia taarifa muda huu kuwa hawataweza kuwasafirisha wagonjwa kwa siku ya leo (Jumamosi) kutokana na hali zao kubadilika, tulitarajia kupokea wagonjwa kama 50 hivi," amesema.

Amesema mpaka sasa tayari Mloganzila imepokea jumla ya wagonjwa 110 mpaka kufikia juzi na wote wapo katika hali nzuri kiafya.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Muhimbili, Aminiel Aligaesha amesema hawajaweza kuhamisha wagonjwa leo kwa sababu hali zao kwa haziruhusu kuwapeleka.

"Ngoja tuwa-stabilize vizuri kisha wataenda wiki ijayo kuanzia Jumatatu. Kumbuka hatuwezi kupeleka wagonjwa wanaoumwa sana ndiyo maana kulingana na hali zao tumeona tusubiri kidogo," amesema Aligaesha.