Wagonjwa wa selimundu walia uhaba wa kliniki

Muktasari:

Wagonjwa hao pia wamelalamikia kukosekana dawa na wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kutoa ushauri na kuwahudumia wanapohitaji huduma.

 Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kupiga vita selimundu iliyoadhimishwa leo (Jumatatu), chama cha wagonjwa wa ugonjwa huo kimelalamikia uhaba wa kliniki maalumu kwa ajili ya kufuatilia maendeleo yao.

Wagonjwa hao pia wamelalamikia kukosekana dawa na wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kutoa ushauri na kuwahudumia wanapohitaji huduma.

Kilio hicho wamekitoa mbele ya Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla wakati wa maadhimisho yaliyoenda sambamba na uzinduzi wa jengo la kituo cha selimundu jijini Dar es Salaam.

Mwanzilishi wa chama hicho, Arafa Salim amesema hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia wagonjwa wengi kukosa huduma.

Amesema upatikanaji wa vipimo na utambuzi wa selimundu umeendelea kuwa changamoto hasa katika maeneo ya vijijini.

Dk Kigwangalla alisema kwa sasa Serikali imeanza utekelezaji wa mpango wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, selimundu ikiwamo.

Amesema kwa kuanzia ameagiza wataalamu waangalie namna gani ambavyo Serikali itaweza kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali zote za wilaya na mkoa.

“Nimeshaagiza wataalamu wafanye utafiti kisha wanipe ripoti ndani ya siku saba wanieleze kwa namna gani tunaweza kuanzisha kliniki hizo nchi nzima ili madaktari wa ugonjwa huu waweze kuwaona wagonjwa, lingine nimetaka waangilie tunavyoweza kutumia kipimo cha haraka kupima selimundu,” amesema.

Dk Kigwangalla ameagiza wataalamu wa selimundu kuanza kufikiria siku moja tiba ya ugonjwa huo ipatikane nchini tofauti na ilivyo sasa matibabu yanapatikana katika mataifa makubwa kama India, Uingereza, Ujerumani na Marekani.