Wahandisi wawapa somo wawekezaji

Mhandisi mkazi wa Kampuni ya OC Global inayojenga daraja la juu la Tazara, Kiyonzi Tsuji (kushoto) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) waliotembelea eneo la ujenzi huo leo. Picha na Ibrahim Yamola


Muktasari:

  • Wito huo umetolewa leo Machi 6, 2018 na wajumbe wa  Bodi ya Usajili wa Wahandisi  waliotembelea ujenzi wa daraja la juu la Tazara jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imewataka wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji wa miradi mikubwa inayotekelezwa hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo Machi 6, 2018 na wajumbe wa ERB waliotembelea ujenzi wa daraja la juu la Tazara jijini Dar es Salaam.

"Ujenzi unakwenda vizuri na wametueleze watakamilisha ujenzi huu Oktoba mwaka huu, lakini tumeshindwa kuchangamkia fursa za kusambaza vifaa vya ujenzi ambavyo tumeshindwa," amesema kaimu msajili wa ERB, Patrick Barozi

Amesema haiwezekani nondo zikatoka nje ya nchi wakati zingeweza kuzalishwa hapa nchini na kuongeza kipato kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.

"Fedha zinazotumika kuagiza nondo Afrika Kusini, saruji ambayo nayo nyingine wanaitoa nje ingeongeza kipato. Kwa hiyo ni wakati sasa kwa wawekezaji kuwekeza katika viwanda ili miradi mikubwa 29 inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano iwanufaishe moja kwa moja Watanzania," amesema Barozi

Awali, akitoa maelezo kwa wajumbe wa ERB, mhandisi mkazi wa Kampuni ya OC Global, Kiyokazu Tsuji amesema mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 80.

Amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni wingi wa magari wakati wa ujenzi, hivyo kuendelea kuziomba mamlaka zinazohusika kusimamia utaratibu wa uongozaji wa magari.