Waitara ashikiliwa polisi kwa kuhoji bomoabomoa

Muktasari:

Taarifa za awali zilizopatikana kutoka kwa dereva wake aliyejitambulisha kwa jina la Koheret Bilage, zimesema kuwa walifika eneo la tukio mchana baada ya kupigiwa simu na wananchi wakisema bomoabomoa ilikuwa inaendelea bila ya wao kupewa taarifa.

Dar es Salaam. Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara ameshikiliwa Kituo cha Polisi Chang'ombe, huku akitakiwa kutoa maelezo kuhusu kuhoji bomoabomoa iliyokuwa ikiendelea eneo la Umoja wa Vijana wa kikristo Tanzania (Uvikiuta), Magole katika Kata ya Kivule.

 

Taarifa za awali zilizopatikana kutoka kwa dereva wake aliyejitambulisha kwa jina la Koheret Bilage, zimesema kuwa walifika eneo la tukio mchana baada ya kupigiwa simu na wananchi wakisema bomoabomoa ilikuwa inaendelea bila ya wao kupewa taarifa.

 

"Waitara nilifika naye pale wakati zoezi linaendelea akahoji kwa kile kikosi cha polisi kwa nini kinabomoa bila taarifa, akaambiwa afike Kituo cha Polisi Chang'ombe, ila tulivyofika akashikiliwa na ili atoe maelezo, lakini alisema hataongea chochote mpaka wakili wake afike," amesema Bilage.

 

Alipotafutwa kwa njia ya simu baadaye, mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa huo amesema alifika kituoni hapo na kushikiliwa na polisi ili atoe maelezo.

 

"Baada ya kuhoji pale polisi waliniambia niende nikamuone mkuu wa polisi Mkoa wa Temeke, nikatii amri kuja huku, ile nafika nikashikiliwa na kutakiwa kutoa maelezo," amesema Waitara.

 

Waitara amefafanua kuwa eneo hilo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu baina ya Uvikiuta na wananchi wanaoishi sehemu hiyo na kwamba kuna kesi iliyofunguliwa awali ambayo iliamriwa kwa wananchi kutakiwa wahame.

 

"Baada ya ile hukumu wananchi waliamua kukata rufaa kipindi ambacho sikuwa kiongozi na rufaa ilikubaliwa ikafunguliwa kesi namba 159 ya mwaka 2013 ambayo bado hatujaona hukumu, leo tunashangaa bomoabomoa inaendelea," amesema.

 

 

Kadhalika, ameutupia lawama uongozi wa eneo hilo kuhusika kuliuza bila ushirikishwaji wa wanachi na kufuata sheria huku akisisitiza kuwa ubomoaji huo aliacha unaendelea bila wananchi kutoa mali zao majumbani.

 

Alipotafutwa kwa simu ili kutolea ufafanuzi wa sakata hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Mroto simu yake imeita bila kupokewa

 

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene amesema tukio alilofanya Waitara ni mwendelezo wa operesheni Ukuta kwa sababu alikuwa anapinga udikteta uliokuwa unafanywa.

 

Makene ameongeza kuwa hakuna sababu kubwa iliyofanya kushikiliwa na polisi.

 

"Ukuta utaendelea kuishi, halikuwa jambo la siku moja. Walidai kuna oda ya Mahakama ila ilipaswa kuonyeshwa kwake akiwa kama mbunge na mwenyekiti wa mtaa, lakini amekamatwa na imechukuliwa kawaida tu. Huu ni uonevu," amesema Makene.

 

Makene amesema kama chama hawajapendezwa na ubomoaji uliofanyika bila kutoa taarifa kwa wananchi na kutaka kutolewa maelezo ya kina kuhusu waliohusika na suala hilo na hati ya kubomoa ilipotoka.