Waitisha harambee kuchangisha Sh73.3 za ujenzi wa kituo cha polisi

Muktasari:

Wakazi hao zaidi ya 2,500 kutoka kaya 350 walikubaliana kuchangia kila mmoja Sh50, 000 ili kufanikisha mpango huo.

Mwanza. Wakazi wa Mtaa wa Majengo jijini Mwanza wamefanya harambee ya kuchangisha Sh73.3 milioni za ujenzi wa kituo cha polisi.

Wakazi hao zaidi ya 2,500 kutoka kaya 350 walikubaliana kuchangia kila mmoja Sh50, 000 ili kufanikisha mpango huo.

Akizungumza kwenye harambee hiyo, mwenyekiti wa kamati ya ujenzi huo, Anthony Jakonyango alisema mtaa huo haujawahi kuwa na kituo cha polisi tangu ulipoanzishwa mwaka 2o12.

 Jakonyango alimpongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi kwa kukubali kituo hicho kujengwa pamoja na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupima sehemu inayofaa kwa ujenzi huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha alisema jukumu lao ni kuhakikisha suala la ulinzi na usalama linaimarishwa kila sehemu.