Wajasiriamali 280 kukutana Pwani

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage

Muktasari:

Maonyesho hayo yanayoratibiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (Sido), yanatarajiwa kuzinduliwa kesho na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage  katika Viwanja vya CCM wilayani humo.

Pwani. Wajasiriamali 280 kutoka mikoa ya Kanda ya Mashariki, wanatarajiwa kushiriki maonyesho ya tisa yatakayofanyika wilayani Bagamoyo, Pwani.  Maonyesho hayo yanayoratibiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (Sido), yanatarajiwa kuzinduliwa kesho na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage  katika Viwanja vya CCM wilayani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amewataka wananchi na wadau kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hao, kwani zimetengenezwa kwa ubora unaotakiwa.

 Meneja wa Sido Mkoa wa Pwani, Agnes Yesaya amesema kaulimbiu ya maonyesho hayo ni ‘Uchumi wa viwanda unategemea viwanda vidogo’. Yesaya alisema lengo ni kukuza ubora wa bidhaa na kujifunza mbinu za ushindani, kusaidia wajasiriamali hasa wa vijijini  kutangaza bidhaa zao.