Wajasiriamali walemavu wamlilia Zitto kuwasaidia

Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Muktasari:

  • Akizungumza leo kwenye maonyesho ya bidhaa mbalimbali zinazotengezezwa na walemavu wanaoadhimisha wiki ya viziwi kimataifa, Mwenyekiti wa Furaha ya  Wanawake wajasiliamali kwa Viziwi Tanzania(Fuwavita), Aneth Gerana alisema wamepata kiwanja  kilichopo Sinza Afrikasana jijini hapa lakini hawana fedha za ujenzi.

Dar es Salaam. Wajasiliamali wenye ulemavu wamemuomba Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe awasaidie kwa kushirikiana na wabunge wengine kuwaunganisha na wawekezaji wa kujenga kiwanda kidogo ili kupunguza tatizo la ajira kwa jamii hiyo.

Akizungumza leo kwenye maonyesho ya bidhaa mbalimbali zinazotengezezwa na walemavu wanaoadhimisha wiki ya viziwi kimataifa, Mwenyekiti wa Furaha ya  Wanawake wajasiliamali kwa Viziwi Tanzania(Fuwavita), Aneth Gerana alisema wamepata kiwanja  kilichopo Sinza Afrikasana jijini hapa lakini hawana fedha za ujenzi.

"Tumewachagua ili mtusaidie tuna changamoto nyingi lakini tunaamini mkitusaidia kupata wawekezaji itatusaidia kuweza kuzalisha bidhaa zetu kwa wingi, tutaongeza idadi ya wenye ajira, lakini pia tutakuwa tumeshiriki katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na tutapunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi," alisema Gerana.

Kabwe ambaye ni Mbunge wa  Kigoma Mjini alisema anajua changamoto zinazowakabili walemavu hasa wanawake kwa kuwa alijionea kwa mama yake mzazi ambaye alikuwa mlemavu, hivyo aliahidi kuwashawishi wabunge wenzake ili kutambua kuwa ni wajibu wa kuwasaidia kwa kuwawezesha kujitegemea.