Balozi Seif awaonya wajumbe Baraza la Wawakilishi

Muktasari:

Amesema kitendo cha baadhi ya wajumbe kutumia ukumbi huo kuchagia kwa kutumia lugha isiyofaa  wanapokosoa Serikali au chama tawala katika michango yao hakileti sura nzuri kwa nchi na jamii kwa ujumla.

Zanzibar. Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuacha mara moja tabia ya kutumia maneno na lugha isiyofaa kwenye vikao vya baraza hilo.
Balozi Seif amesema hayo leo Ijumaa katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati akitoa hotuba ya kuairisha mkutano wa tisa wa baraza hilo la saba.
Amesema kitendo cha baadhi ya wajumbe kutumia ukumbi huo kuchagia kwa kutumia lugha isiyofaa  wanapokosoa Serikali au chama tawala katika michango yao hakileti
sura nzuri kwa nchi na jamii kwa ujumla.

“Sisemi hivi kwa sababu ya kuwafunga mdomo wajumbe kuikosoa Serikali hapana mnao uhuru wa kufanya hivyo lakini ni vyema kutumia lugha nzuri zaidi ili jamii ione kazi tunayofanya wajumbe wao waliotuchagua,’’amesema Balozi Seif.

Amesema ni busara zaidi wajumbe wa chombo hicho cha kutunga sheria kuendana na mila za waZanzibar ikiwa ni pamoja na kutumia lugha nzuri ili vikao vya baraza hilo viendelee kuwa chem chem ya kuleta matumaini kwa jamii inayofatilia.

Hata hivyo Balozi aliwataka wananchi visiwani hapa kuendelea na shughuli zao kama kawaida na kuondoa kabisa dhana ya uwepo wa mabadiliko katika safu ya uongozi wa nafasi ya Rais.

Amesema uchaguzi umekwisha na Dk Mohammed Shein ndiyo kiongozi wa Serikali ya Zanizbar hadi kumalizika kwa miaka yake mitano ya uongozi wa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

“Niwaombe wananachi waendelee na kazi zao kama kawaida wala wasiwe na hofu wakijua kuwa Dk Shein ni kiongozi na ataendelea kuwepo kwa muda wa miaka mitano,” amesema.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuachana kabisa na suala la magendo ya karafuu kwa kuwa kufanya hivyo ni kuikosesha Serikali mapato ambayo yalitakiwa kutumika ndani ya Zanzibar kwa maendeleo ya wananchi wake na Taifa kwa ujumla.