MKUTANO MKUU CCM: Wajumbe Nec wataka Rais Magufuli aifumue CCM

Muktasari:

Kikao hicho jana kilipitisha jina la Rais John Magufuli kuwa mgombea pekee wa nafasi ya mwenyekiti wa CCM katika uchaguzi utakaofanyika leo, kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka.

Dar/ Mikoani. Siku moja kabla ya Rais John Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, wenyeviti na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wamemtaka kufanya mabadiliko makubwa ya kukisaficha chama.

Kikao hicho jana kilipitisha jina la Rais John Magufuli kuwa mgombea pekee wa nafasi ya mwenyekiti wa CCM katika uchaguzi utakaofanyika leo, kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka.

Makada walioulizwa na Mwananchi swali la “wanataka Magufuli aifanyie nini CCM, wengi wamemtaka aondoe makundi yaliyopo kwenye chama na baadhi wakitaka akisafishe kwa kushughulikia mafisadi na watendaji wasio waaminifu.

Mjumbe wa Nec kutoka Zanzibar, Suleiman Sarhan alisema baada ya Rais Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti atapenda aanze na mabadiliko ndani ya chama ili kuwashughulikia watendaji wote ambao si waaminifu.

“Watendaji siyo waaminifu na si watendaji. Wengine wamechoka lakini pia wapo waliolewa madaraka na kujisahau. Wengine wanafanya vitendo vya rushwa na kifisadi. Hatuwezi kwenda hivi katika chama, ni lazima tusafishe chama chetu,” alisisitiza Sarhan.

Sarhan alisema pia mwenyekiti anapaswa kurudisha mshikamano ambao ulionekana wazi kuanza kutoweka ndani ya chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Antony Diallo amemtaka mwenyekiti mpya kusafisha mfumo uliokuwapo ambao ulitoa fursa ya kuwa na watendaji wengi, jambo ambalo linaongezea matumizi makubwa yasiyo na msingi.

“Ni lazima tupunguze idadi ya watendaji katika chama chetu. Wafanyakazi wamekuwa wengi na kukielemea chama, lazima tubane matumizi ili kuendana na hali halisi ya sasa,” alisema Diallo.

Mjumbe kutoka Sumbawanga, Aeshi Hilaly alisema ukweli ni kwamba chama kilijeruhiwa na kuumizwa sana na wasaliti na kwamba licha ya kupitisha jina la mtu katika nafasi mbalimbali, wasaliti hao hawakuwaunga mkono jambo lilosababisha ugumu katika uchaguzi.

“Watu walifanya makosa hawakushughulikiwa jambo lililosababisha manung’uniko kila kona. Hili ni lazima tulikomeshe sasa,” alisema na kuongeza kuwa lazima mwenyekiti ahakikishe nidhamu inarudi katika chama na kurudisha mshikamano uliokuwapo.

Mjumbe mwingine kutoka Zanzibar, Faida Mohamed Bakari alisema Rais Magufuli ana kazi kubwa ya kuunganisha wanachama kwa kuwa hali ilishakuwa mbaya baina ya wanachama, lakini pia avutie ambao hawapo CCM kujiunga na chama ili kuongeza wigo.

“Lazima tukubaliane kuwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliacha makovu makubwa ndani ya chama hivyo lazima yazibwe,” alisema Faida.

Hata hivyo, Faida alisema katika kuziba makovu hayo mwenyekiti hana budi kufuata viwango, uvumilivu na ubunifu aliokuwa nao mwenyekiti aliyepita, Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa Faida, Rais Magufuli tayari ameshaonyesha serikalini kwamba anaweza, anaamini hata chama hakitamshinda. Alisema jambo la msingi ni kutosahau kuchota uzoefu wa viongozi waliomtangulia kwa kuwa watampa mawazo yatakayosaidia kukiimarisha chama.

Katibu wa siasa na uenezi wa Mkoa wa Dodoma, Donald Mejitii alisema wanatarajia aendeleee kuimarisha uhai wa chama ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kinakuwa na uadilifu wa hali ya juu.

“Apiganie kuhakikisha kuwa hakuna rushwa katika uchaguzi wa ndani ya chama na vyombo vya dola. Ahakikishe nafasi za utendaji wa chama ziwe za haki,” alisema.

Pia, alimtaka mwenyekiti huyo kuhakikisha anasimamia watendaji wa chama ili wapate nafasi na kupanda madaraja kwa haki kwa kuzingatia utumishi wake na uadilifu ndani ya chama.

Mbunge wa Mtera ambaye anaingia Halmashauri Kuu kwa nafasi yake, Livingstone Lusinde alisema kwa nafasi aliyonayo Rais Magufuli anajua katiba inamtaka afanye nini baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti.

“Lakini watu watarajie mambo makubwa katika uongozi wake ni lazima mambo yatabadilika kwa lengo la kukiimarisha chama,” alisema.

Naye Evod Mmanda alisema kwa ujumla chama hakina kipaumbele zaidi ya Ilani ya Uchaguzi, hivyo amemshauri mwenyekiti mpya kuisimamia ili kuhakikisha mipango ya chama na Serikali inaenda vizuri.

“Lakini pia aimarishe safu ya uongozi kutoka ngazi ya chini mpaka juu na kusimamia majukumu yake. Chama kitakuwa katika wakati mzuri,” alisema.

Mjumbe mwingine kutoka Hanang, Mary Nagu alimtaka Magufuli akiunganishe chama ili wawe wamoja.

Hivi karibuni katibu wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Dodoma kuwa Rais Magufuli ana kazi kubwa ya kutumbua majipu ndani ya chama hicho kwa sababu yapo mengi.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Idd Juma alisema angependa Rais Magufuli aanze na kazi ya kukijenga chama hicho ili kiweze kuwa na uchumi imara kwa kuviimarisha vitega uchumi iliyonavyo.

“Naamini Rais Magufuli atakifanya chama kiwe imara na naamini ushirikiano ambao ataupata kutoka kwa wanachama atafanikiwa ila nataka sana akiimarishe chama kiuchumi,” alisema Juma. Mwenyekiti huyo alisema ni vyema Rais Magufuli akakiimarisha chama kiuchumi ili miradi na vitega uchumi ilivyonavyo ikiwezeshe kuwa chama imara kiuchumi kisichotegemea ruzuku.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Lindi, Ali Mtopa alisema Magufuli arudishe utaratibu wa enzi za Tanu wa kuwalipa posho wakuu wa mikoa wanaojitolea kujijenga chama.

“Kuna watu hawa wakuu wa mikoa wanajitolea kufanya kazi za chama , naomba walipwe posho kama vile ilivyokuwa wakati wa Tanu. Hilo tu,” alisema. “Lakini nataka aendelee na hii kazi hii (kupambana na ufisadi) ambayo imemfanya hata watoto wadogo wanamfahamu. Tena akiwa na kofia mbili ndiyo ataifanya kwa uzuri.”

Mwenyekiti wa CCM wa Moshi Mjini, Elizabeth Minde alisema anatamani Rais Magufuli anapokabidhiwa uenyekiti leo, aanze na kazi ya kukisafisha chama kama anavyofanya serikalini.

“Ningetamani aanze kusafisha chama kama anavyosafisha serikalini ili kitulie na kichukue nafasi yake kama chama bora kinachoongoza taifa kubwa. Tuwe na wanachama na viongozi waadilifu,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM wa Arusha, Lekule Laizer alisema kazi ya kwanza ambayo mwenyekiti mpya anatakiwa aifanye ni kupanga safu nzuri ya uongozi itakayoendana na kasi yake.

Lekule alisema wana imani Rais Magufuli ataondoa makundi ndani ya CCM na hivyo kurejesha umoja na mshikamano. “Kama alivyofanya kwenye Serikali tunaamini pia atateua sura mpya ambazo zitasaidia kukiimarisha chama chetu,” alisema.

Lekule, ambaye alichaguliwa karibuni kushika nafasi ya Onesmo ole Nangole aliyehamia Chadema, alisema mkoa huo una imani kubwa na Magufuli.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msavatavangu pia alimshauri Rais Magufuli akiimarishe chama hicho kikongwe barani Afrika kiuchumi na aanze kuachia pesa ziingie katika mzunguko halali wa kiuchumi ili Watanzania wakiwamo wana CCM waanze kunufaika na mzunguko huo.