Wakati maambukizi ya ukimwi yakishuka, wanandoa walioachana waingia hatarini

Muktasari:

Billingi anasema utafiti huo kwa mara ya kwanza umewashirikisha watoto wadogo.


Kwa miongo mitatu mfulululizo ugonjwa wa ukimwi umekuwa tishio nchini na duniani kutokana na kushindwa kupata dawa yake.

Hata hivyo, kumekuwapo na harakati kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chanjo ya ugonjwa huo inapatikana ili kujikinga na maambukizi hayo na kwa wale walioathirika wamekwa wakipatiwa dawa za ARV’s kwa ajili ya kufubaza virusi hivyo.

Nchini Tanzania Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), imekuwa ikiongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huo toka mwaka 2007 ambako maambukizi yalifikia asilimia 7.5 lakini sasa juhudi za mapambano hayo yanaonekana.

Hivi karibuni tume hiyo imefanya utafiti wa kitaifa wa viashiria na matokeo ya ukimwi kwa mwaka 2016/17 na kutoa ripoti yake ambako matokeo yanaonyesha kuuwa wanandoa waliotalikiana wanaoongoza kwa asilimia 11 kuwa na maambukizi ya VVU.

Ripoti hiyo iliyosomwa mbele ya wahariri wa vyombo vya habari mjini Bagamoyo mapema wiki hii inaonyesha wanandoa nao wanapata maambukizi ya VVU kwa asilimia 4.8.

“Hakuna sababu moja maalumu ya wanandoa au waliotalikiana kuwa na maambukizi kwa kiasi kikubwa kwani zipo sababu nyingi,”anasema mratibu wa Tacaids Mkoa wa Tanga, Juma Billingi

Awali, akizungumzia hali ya maambukizi, Billingi alisema: “Watanzania 81,000 wanapata maambukizi mapya kila mwaka sawa na asilimia 9.2.”

Anasema mkoa unaoongoza kwa maambukizi ni Njombe wenye asilimia 11.4 ukifuatiwa na Iringa (11.3) huku mkoa wa mwisho wenye kiwango kidogo ukiwa ni Lindi (0.3).

Kuhusu kitaifa, Billingi anasema kwa sasa kiwango cha maambukizi nchini ni asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 5.1 miaka minne iliyopita.

Anaongeza kuwa huo ni utafiti wa tatu kufanywa na Tacaids ambao unafanywa kila baada ya miaka minne.

Alisema wa kwanza ulifanyika 2007/08 na kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 7.5.

“Wa pili ulifanywa 2011/12 na matokeo yalionyesha kiwango kilikuwa 5.1 na sasa 2016/17 ndiyo hiyo asilimia 4.7,”anasema.

Hata hivyo, mratibu huyo anasema takwimu hizo ni himilivu kwa sababu hazipungui wala kuongezeka na kiwango cha maambukizi si kikubwa.

Anasema kiwango cha maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.2 ukilinganisha na wanaume ambayo ni asilimia 3.1

Wakazi wa mijini waongoza kwa maambukizi

Anasema takwimu zinaonyesha kwamba kiwango cha maambukizi kwa wanawake wanaoishi mjini ni asilimia 7.8 wakati wanaume ni asilimia 2.8.

Hata hivyo, anasema makundi yaliyo hatarini zaidi kupata VVU ni wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanaofanya biashara ya ngono na watu wa mipakani.

Sababu za kuwapima watoto

Billingi anasema utafiti huo kwa mara ya kwanza umewashirikisha watoto wadogo.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, chanzo cha kuwapima virusi vya ukimwi watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi 14 ni baada ya utafiti kuonyesha kundi hilo linaanza kujamiiana likiwa kuanzia miaka 10 na kuendelea.

“Utafiti wa sasa umehusisha kwa mara ya kwanza watoto kuanzia miaka 0 mpaka 14; 14 hadi 49; na 50 na kuendelea,” anasisitiza Billingi.

Akizungumzia watoto kuanza kujamiina wakiwa na umri mdogo, ofisa utafiti wa Tacaids, Dk Arodia Mulokozi anasema: “Wanafunzi wengi ni wanafunzi mchana tu usiku balaa tupu.”

Dk Mulokozi anasema baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu ndiyo wapo hatarini zaidi hasa wanapofika mwaka wa pili.

“Hatari zaidi wakiingia mwaka wa kwanza wapolee wakifika wa pili siyo wale tena wengi wanapata ujauzito ina maana hawatumii kondomu.”

Matokeo ya homa ya ini

Utafiti huo wa ukimwi uliohusisha pia matokeo ya homa ya ini kwa mwaka 2016/17 umeonyesha kuwa ugonjwa wa homa hiyo (Hepatitis B) unawashambulia zaidi waishio maeneo ya mijini kuliko vijijini.

Billingi anasema kwa upande wa Tanzania bara, wenye umri wa miaka 15 na zaidi wanaoishi maeneo ya mijini wameathirika zaidi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini kwa asilimia 4.3.

“Hiyo ni ongezeko kubwa kuliko walioko vijijini ambao wameathirika kwa asilimia 3.3 kwa mijini asilimia 4.2 ni wanawake na 4.4 ni wanaume.”

Anasema katika utafiti huo pia umeonyesha waliopo kwenye ndoa au kuishi pamoja maambukizi yao yapo juu ikilinganishwa na wasiokuwepo ndoani.

Mkakati wa kudhibiti Ukimwi

Wakizungumzia mkakati wa nne wa kudhibiti Ukimwi nchini NMSF-IV, tume hiyo inasema umezingatia kupitishwa kwa mbinu mpya ikiwemo kinga ya maambukizi (PrEP, PEP), upimaji binafsi na uboreshwaji wa huduma za matibabu kwa waishio na virusi.

Kwa mujibu wa Dk Mulokozi, mkakati huo ni matokeo ya kina ya tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa tatu 2013/14-2017/18 ambao upo katika hatua za mwisho kiutekelezaji umelenga kuhakikisha wote wanaopimwa na kukutwa na VVU asilimia 2.8 wanaunganishwa na huduma za tiba na matunzo.

“Kwa wale wote ambao watakutwa hawana maambukizi tunakadiria asilimia 97.2 wanaingizwa katika mipango ya kitaifa ya kudhibiti maambukizi kupitia uhamasishaji, habari na elimu katika kuzingatia tabia zisizo za hatarishi.

Anasema malengo ya mkakati huu ni kupungua kwa maambukizi mapya kwa asilimia 75 ifikapo 2020 na kwa asilimia 85 kufikia mwaka 2023.

Anaongeza kuwa mkakati huo umedhamiria kupunguza vifo vitokanavyo na ukimwi kwa asilimia 50 ifikapo 2020 na kwa asilimia 75 ifikapo 2023 na asilimia 80 ifikapo 2030.

“Katika maambukizi kutoka kwa mama na mtoto mkakati huu umedhamiria kupungua kwa asilimia 5 ifikapo 2023 na asilimia 2 ifikapo 2030 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo 2030,” anasema.

Dk Mulokozi anasema pia unalenga kuongeza idadi ya watu wanaojua hali zao za maambukizi, ubunifu kwa kutumia njia mbali mbali za kupima VVU – PITC, huduma za kliniki kupitia magari (mobile clinics), kujipima mwenyewe na kupima kwa kulenga makundi hatarishi.

Pia, kuongeza na kuimarisha rufaa katika tiba na matunzo kwa wenye virusi na kutoa elimu ya lishe bora na misaada kwa wasiojiweza, huduma za hiari za tohara za kitabibu kwa wanaume na upatikanaji wa huduma za tohara.

“Uhamasishaji wa matumizi sahihi ya kondomu, kinga dhidi ya virusi vya ukimwi (PrEP) kwa kuimarisha huduma za ushauri na upimaji- HTS na upatikanaji na utoaji wa ARV kama kinga kwa makundi maalumu (KVPs).”

‘Furaha yangu’

Akizungumzia kampeni hiyo yenye lengo la kusaidia kuongeza kasi na uimarishwaji wa afua zenye matokeo makubwa ili kuzuia maambukizi mapya ya VVU na kupunguza vifo vinavyotokana na UKIMWI (90-90-90 ifikapo mwaka 2020) mkurugenziwa Utetezi na Mawasiliano Tacaids Jumanne Isango anasema tayari kampeni hiyo inatekelezwa katika mikoa 19.

“Malengo ni kuongeza ufanisi na ushiriki wa kimkakati wenye tija kutoka kwa wadau wote, na hasa jamii katika utekelezaji wa mwitikio shirikishi wa kitaifa wa kudhibiti Ukimwi.”