Wakazi 2005 wanaopisha ujenzi wa Ikulu waanza kulipwa leo

Muktasari:

  • Kuna wakaazi 2719 waliopisha ujenzi wa Ikulu wanaotakiwa kulipwa lakini kwa leo watalipwa wakazi 2005 na malipo kwa wengine yataendelea.

Dodoma. Wakazi 2005 wa Wilaya za Chamwino na Dodoma Mjini mkoani Dodoma wanaopisha upanuzi wa Ikulu wameanza kulipwa fidia leo Septemba 11, 2018.

Mkurugenzi wa Miliki wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA) Baltazar Kimangano amesema  jumla ya wakazi 3191 wanatakiwa kupisha upanuzi wa Ikulu na kwamba awamu ya kwanza iliyofanyika Desemba mwaka jana ilianza na wakazi 471 wa maeneo hayo.

Amesema wakazi waliobaki ni 2719 na kwamba leo watalipwa 2005 baada ya udhamini kukamilika na hivyo watabaki 714 ambao udhamini wao unaendelea.

 “Tumetenga Sh 7bilioni kwa ajili ya kuwalipa wakazi wote watakopisha upanuzi huo. Na katika awamu hii tutalipa Sh 5.3 bilioni,”amesema.

Amewataka wakazi wa vijiji vya Buigiri, Malecela, Kalama, Mwongozo, Vikonje na Chavuma kujitokeza kuchukua hundi zao.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema wakati anaingia ofisini miongoni mwa changamoto alizokutana nazo ni malalamiko ya wananchi juu ya ulipaji wa fidia katika maeneo yao yaliyochukuliwa kwa ajili ya Ujenzi wa Ikulu na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege.

“Sasa kabla ya mwaka kumalizika Serikali imetafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo ni hatua kubwa ambayo Rais anapaswa kupongezwa. Rais amedhamiria kwa vitendo kuhakikisha Dodoma inakuwa makao makuu ya nchi,”amesema.