Tuesday, September 11, 2018

Wakazi 60 waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege Dom waanza kulipwa leo Mkurugenzi Mkuu wa TAA Richard Mayongela

 Mkurugenzi Mkuu wa TAA Richard Mayongela 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) leo Septemba 11, 2018, imeanza kuwalipa fidia wakazi 60 wa Chadulu B  Wilaya ya Dodoma Mjini ambao wanapisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege.

 Mkurugenzi Mkuu wa TAA Richard Mayongela amesema kuwa  jumla ya Sh 3.392 bilioni zitatumika kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi hao ambao walifanyiwa tathimini mwaka 2016.

Amesema tayari Sh 2.1bilioni zimetumika kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi wa eneo hilo katika awamu ya kwanza na kwamba awamu ya pili itakayohusisha ulipaji wa Sh 3.392 bilioni imeanza leo.

Amesema wakati wanafanya tathimini mwaka 2016, gharama ya kuwalipa watu wote watakaopisha upanuzi huo wenye ukubwa wa urefu wa mita 530 ilikuwa ni  Sh 13 bilioni.

“Mkakati wetu tutaendelea kufidia kwa wakazi waliobakia ili tuweze kuweka taa. Mfumo wa taa ambao utawekwa hapa unaitwa simple Approach Light System. Ni ule mfumo ambao kazi yake ni kumsaidia rubani anapoteremka, unamuongoza hapa sasa anza kuteremka,”amesema.

Amesema hiyo ni muhimu kwasababu tayari viongozi wakuu wamehamia Dodoma na hivyo kuweka ulazima wa kuwa na kiwanja cha ndege ambacho kitafanya kazi saa 24.

Amesema kuwa fedha zilizotumika kuwalipa wakazi hao zinatokana na vyanzo vya ndani kwa mamlaka hiyo.

-->