Wakazi Dodoma wahofia kukumbwa na magonjwa

Muktasari:

Mabwawa hayo yanayopokea majitaka kutoka katika maeneo mbalimbali yakiwamo hospitali, viwandani na majumbani yanamilikiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa).

Dodoma. Baadhi ya wakazi wa Dodoma wameonyesha hofu ya kukumbwa na magonjwa kutokana na mboga nyingi zinazouzwa katika masoko kuzalishwa kwa kutumia majitaka kutoka katika mabwawa ya Swaswa.

Mabwawa hayo yanayopokea majitaka kutoka katika maeneo mbalimbali yakiwamo hospitali, viwandani na majumbani yanamilikiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa).

Mkazi wa Mailimbili, Scolastica Bernad aliiomba Serikali kufanya utafiti kuhusiana na mboga hizo ili kuwaepusha walaji kukumbwa na magonjwa hayo.

“Serikali imetangaza kuhamia Dodoma ni vyema sasa katika mipango yao ya maandalizi ukafanyika utafiti wa ubora wa mboga zinazozalishwa kwa kutumia maji hayo. Na hiki kimekuwa ni kilio chetu cha muda mrefu,” alisema.

Akizungumza katika kikao cha ushawishi wa lishe baina ya viongozi wa Serikali na wadau wa lishe, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Dodoma, Mary Boniventure aliungana na wakazi wa mji huo kuonyesha hofu ya maji yanayotumika kumwagilia bustani katika eneo hilo la Swaswa.

“Maji machafu yote yanayotoka hospitalini, viwandani na majumbani yanakwenda katika mabwawa hayo (Swaswa). Ndiyo maji yanayotumika kumwagilia mboga,” alisema.

Alisema nchi nyingine wanatumia majitaka baada ya kuyatibu na wana mfumo wa umwagiliaji wa matone ambao maji yanakwenda moja kwa moja yanapohitajika tofauti na eneo hilo wakulima humwagilia hadi kwenye majani, matunda na mboga.

Aliwashauri wakazi wa mkoani hapa kulima mboga kwenye nyumba zao ili kuepuka kutumia vyakula wasivyofahamu vilivyozalishwa.

“Sasa huku wanachota maji kwa kutumia chombo, yanakwenda moja kwa moja katika mboga za majani zinazochumwa. Tujiongeze, mboga tuzilime wenyewe nyumbani kwetu,” alisema.

Aidha, alisema tatizo la usalama wa chakula haliko kwenye mboga pekee bali hata kwa nafaka kulingana na utayarishwaji wake.

Alisema ni vyema walaji wa unga wa dona wakanunua mahindi na kuyachumbua, kusafisha kabla ya kusaga ili kuondoa nafaka zilizoharibika.

Mkurugenzi wa asasi ya Alpda, Jacob Wassena alisema hofu ya usalama wa maji hayo imeanza kuzungumzwa siku nyingi, lakini bado hatua za kufanya uchunguzi hazijachukuliwa. Alishauri ifike mahali hatua zichukuliwe.

“Sasa Serikali inakuja kuhamia Dodoma hebu tufanye utafiti wa jambo hili kama mboga hizi zina madhara ama la maana suala hili limeanza kuzungumzwa siku nyingi,” alisema Wassena.

Alisema karibu katika kila zahanati ugonjwa unaozungumziwa ni Typhoid, ni vyema ukafanywa utafiti wa kina ili kujua kama kuna madhara ambayo wanapata watu wanaotumia mboga hizo.

Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Cosmas Ngafa alisema wataalamu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) cha mkoani Morogoro, wamewahi kufanya utafiti wa usalama wa majitaka katika kilimo na kugundua athari zake kiafya ni kubwa.

Hata hivyo, alisema ni vyema mkoa na Duwasa wakaangalia usalama wa maji hayo ili kuepuka madhara kwa watumiaji wa mboga hizo.

Alitoa mfano wa bwawa la Mindu ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikiwa na baadhi ya wakazi wa wa Morogoro ubora wa maji yake.

“Ndiyo maana kipindupindu hakitoki pale (Morogoro) kimeendelea kung’ang’ania na kimesambaa katika wilaya nyingine za mkoa huo,” alisema.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa ya Dodoma, Dk Joseph Mdachi alisema inategemea na maji yanayotumiwa na wakulima wa mboga hizo.

Alisema maji yanayotoka moja kwa moja kwa watumiaji na kuingia kwenye mabwawa ndiyo yana madhara katika kilimo na si yale ya mwisho.

Kuhusu Dodoma kuwa na wagonjwa wengi wa Typhoid, Dk Mdachi alisema vifaa vya kuweza kugundua maradhi hayo ni vichache kwa manispaa hiyo.

“Vifaa vya kugundua Typhoid ni vichache Dodoma. Hivyo ndivyo vinavyoweza kumhakikishia mtu anaumwa ugonjwa huo au la.

“Hospitali ya Rufaa Dodoma, Hospitali ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe na Kituo cha Afya cha Makole wanavyo vifaa vya kupima na kugundua,”alisema.

Meneja Mawasiliano wa Duwasa, Sebastian Warioba alisema maji yaliyo katika mabwawa hayo yanakuwa yametibiwa hivyo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.

“Maji haya ni mengi yanayotoka katika outlet yanakuwa salama kwa kilimo kwa kuwa yanakuwa yameshafanyiwa nature treatment (yametibika) hayana madhara kwa kilimo,” alisema.

Alisema majitaka katika mabwawa hayo yamekuwa yakifanyiwa vipimo vyamara kwa mara katika maabara ya kisasa ya Duwasa iliyopo Mbwanga mjini hapa.

Alisema licha ya wao kufanya uchunguzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imekuwa ikichukua sampuli ya majitaka na majisafi mara kwa mara na kuonekana ni salama.

“Unajua Dodoma bado hatuna viwanda vinavyozalisha kwa kemikali kama ilivyo kwa Dar es Salaam na kwingineko, kwa hiyo hata maji yakipimwa hayaonyeshi kemikali,” alisema.

Hata hivyo, alisema wakulima wachache wamekuwa wakiyatumia maji ambayo bado hayajatibiwa kwa kilimo cha umwagiliaji.

“Tumetoa elimu kwao na tunaendelea kutoa elimu mara kwa mara kupitia redio na mikutano katika eneo hilo, lakini bado wapo wachache wanaoendelea kutumia na polisi wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua,”alisema.

Katibu Ofisa Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba alitaka elimu ya kinga dhidi ya magonjwa kupewa umuhimu kwa sababu kutibu ni gharama kubwa kuliko kinga magonjwa.

Alitoa mfano wa ugonjwa wa sumukuvu uliojitokeza mkoani Dodoma ambao unasababishwa na kula vyakula vilivyo na sumu hiyo na kusababisha vifo vya watu 16.

Alisema tatizo hilo ni chanzo cha udumavu katika jamii na kutaka wadau wa lishe kushiriki kutoa elimu juu ya kuepuka ugonjwa huo.

Alisema udumavu umekuwa tatizo kubwa na kuathiri uchumi wa kaya, jamii, uelewa na watoto shuleni, uzalishaji viwandani na kushuka kwa pato la Taifa.

Alisema hali hiyo inadhihirishwa mkoani Dodoma ambako tatizo la udumavu limebainika.

Kitaifa takwimu zinaonyesha tatizo hilo liko kwa asilimia 56, uzito pungufu asilimia 16 na ukondevu asilimia tano na upungufu wa viini lishe.