Tuesday, January 9, 2018

Wakazi Vunjo wabebeshwa zigo la barabara

 

By Janeth Joseph, Mwananchi Jjoseph@Mwananchi.co.tz

 Zaidi ya Sh200 milioni zinatarajiwa kutolewa kwa kata nne za Vunjo katika harakati za kuchangia matengenezo ya miundombinu ya barabara.

Katibu wa mbunge Jimbo la Vunjo, Danielson Shayo alisema kila kaya itachangia Sh 20,000 wakati wenye uwezo watachangia zaidi.

Alisema kata nne kubwa katika jimbo hilo zitachangia kiasi hicho cha fedha kutokana na idadi kubwa ya vijiji na vitongoji.

Alizitaja kata hizo kuwa ni Marangu Mashariki, Magharibi, Kirua Vunjo Magharibi na Makuyuni ambazo zina idadi kubwa ya vijiji na vitongoji.

“Katika kata hizo kila kaya itachangia Sh20,000 na wenye uwezo tumewatumia barua ili kuwaomba mchango wao zaidi,” alisema.

Hata hivyo, alisema baada ya kongamano la Novemba 20, 2017 walikutana na viongozi wa vijiji na watendaji ili kuangalia jinsi wananchi watakavyochangia fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

“Kuanzia Januari, mwaka huu mbunge wa jimbo hili James Mbatia atatembelea ofisi za kata hizo ili kuangalia watu wamepokeaje suala hilo la maendeleo na kwa siku atatembelea kata tano katika jimbo hilo lenye kata 16,” alisema Shayo.

Katika barua yake ya Desemba 11, Mbatia alieleza kuwa katika kongamano hilo walikubaliana kila mwana Vunjo atachangia fedha kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu na wadau wengine wa maendeleo ndani na nje ya jimbo.

“Kutokana na andiko la Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Jimbo la Vunjo lina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 272.8 ikijumlisha barabara zote katika vijiji 78 na vitongoji 18 vya Mji Mdogo wa Himo,” ilieleza barua hiyo.

Katika makisio yaliyofanywa na ofisi ya mbunge huyo Sh7.29 bilioni zinahitajika kufanya matengenezo ya barabara ambapo mitambo inakisiwa kugharimu zaidi ya Sh4 bilioni (sawa na asilimia 56) ya gharama za mradi.

Barua hiyo ilieleza kuwa, uendeshaji wa mradi huo utagharimu zaidi ya Sh3 bilioni (sawa na asilimia 44) zinazotakiwa zipatikane kwa kushirikiana na wakazi wa jimbo hilo wanaoishi ndani na nje ya Vunjo.

“Kila kata itapewa namba maalumu zitakazotumiwa kuona ushiriki wa kila mmoja katika uchangiaji lengo likiwa ni kuonyesha uwazi na uwajibikaji wakati wote wa zoezi hilo,” ilieleza barua hiyo.

Mkazi wa Kijiji cha Kiraracha, Haika Mandara alisema wapo tayari kumuunga mkono mbunge kwa kuwa miundombnu hiyo itasaidia kurahisisha mawasiliano na huduma za kijamii kufikika.

-->