Wakazi wa Ulongoni A waomba kujengewa daraja

Muktasari:

  • Wameeleza kilio chao leo katika  ziara ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, Jumanne Shauri aliyetembelea Ulongoni A  kujionea hali halisi ya ubovu wa daraja hilo

Dar es Salaam. Wakazi wa Ulongoni A jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali kujenga daraja katika eneo hilo baada ya lililokuwa awali kubomoka na kusababisha adha ya usafiri.

Wameeleza kilio chao leo Jumamosi Septemba 22, 2018 katika  ziara ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, Jumanne Shauri aliyetembelea eneo hilo kujionea hali halisi ya ubovu wa daraja hilo.

Shauri akiwa ameambatana na katibu tawala wa halmashauri hiyo, Sheila Edward, wameshuhudia  namna watembea kwa miguu wanavyopita eneo hilo kwa tabu pamoja na magari ambayo baadhi yalizimika katikati ya maji.

Amesema halmashauri  imejipanga kufanya tathmini ndani ya mwezi mmoja ili kujua gharama halisi ya ujenzi wa daraja hilo.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Nurdin Kaniki amesema tangu daraja hilo  kubomoka katika msimu uliopita wa mvua wamekuwa wakipata adha ya usafiri ikiwemo kuharibika kwa magari yao.

Mwananchi mwingine, Ziada Hassan amesema akina mama wanaokwenda hospitali  Gongo la Mboto wanapata tabu, hasa kupita katika daraja hilo.