Wakenya watunga wimbo kumuenzi Kanumba

Muktasari:

Wakenya hao wameamua kufanya hivyo ili kumuenzi staa huyo wa filamu aliyefariki dunia miaka sita iliyopita


Dar es Salaam. Steven Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 na katika kukumbuka mchango wake katika uigizaji wa filamu mashabiki wake kutoka Kenya wapo nchini Tanzania kutengeneza wimbo maalumu kwa ajili ya kumbukumbu ya kifo cha muigizaji huyo.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumamosi Machi 24, 2018 kiongozi wa msafara huo, Paul Leonard amesema wamelazimika kufanya hivyo kama njia ya kumuenzi msanii huyo aliyeipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika tasnia ya filamu.

Leonard amesema wimbo huo utakaopewa jina la ‘Kanumba amerudi tena’ wameufanya kwa kushirikiana na wasanii na watayarishaji muziki kwa gharama zao wenyewe, mbali na kurekodi audio, pia watafanya na video ya wimbo huo.

Amesema wakimaliza kuuandaa watamkabidhi mama mzazi wa muigizaji huyo ili aweze kufaidika na mapato yatakayopatikana kokote utakapopigwa.

Alipoulizwa nini kimewasukuma kufanya hivyo, amesema wamekuwa wakifuatilia filamu tangu kifo cha Kanumba na kubaini jambo kama hilo halijawahi kufanywa, hata na waigizaji wa filamu nchini ‘Bongo Movie’.

“Yaani tunashangaa kwanini wasanii wa Bongo wamekuwa wazito kumuenzi msanii huyu ambaye alituwakilisha vema wana Afrika Mashariki, ikiwemo kumtenga mama hata pale anapoenda kuwaomba msaada wa kumsaidia kutengeneza filamu,”amesema.

Katika video ya wimbo huo mbali na wasanii wengine pia watawashirikisha waliowahi kufanya kazi na Kanumba akiwemo Patrick na Jenifer aliocheza nao katika filamu ya This is It na Uncle JJ, iliyofanya vizuri sokoni.

Akizungumzia namna Kenya walivyokuwa wanamchukulia Kanumba, Leonard amesema ni msanii waliyempenda kwa kuwa hakuwa tu anaiwakilisha Tanzania bali na nchi za Afrika Mashariki.

Kwa upande wake mama Kanumba, Flora Mtegoa amesema mashabiki hao wamempa butwaa na kujiuliza Kanumba alikuwa nani hadi afanyiwe yote hayo.

Amesema mbali na Wakenya tayari kuna watu kutoka Oman walishawahi kumtembelea na hapo alipo ana tiketi ya kwenda nchini humo kwenda kupumzika kwa siku kadhaa.

Kanumba alifariki miaka sita iliyopita baada kutokea sintofahamu kati yake na aliyekuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael maarufu Lulu.