Wakesha kusubiri miili

Muktasari:

Mamia ya watu wamekesha huku wakipigwa na baridi kali wakisubiri miili ya ndugu zao.

Ukerewe. Zaidi ya watu takribani 1,200 usiku wa kuamkia leo wamejikuta wakilala macho wakisubiri kuitambua miili ya ndugu zao waliofariki dunia kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

 

MCL DIGITAL imeshududia wananchi hao wakiwa wamejikunyata kando mwa eneo la tukio, huku wakiwa wameelekeza macho yao ziwani.

 

Paulina Nguzu (63) kutoka Bariadi mkoani Simiyu ambaye hadi asubuhi hii hajafanikiwa kumuona mtoto wake wa kiume, anasema anatumaimi kupata mwili wa mtoto wake leo na kuondoka kwa ajili ya maziko.

 

"Kiukweli kuhusu baridi hilo haitusumbui hata kama ni malaria kutokana na mbu, tutaenda hospitali, cha msingi ni kukabidhiwa mwili wa mtoto wetu tuondoke kama wenzetu waliotangulia," amesema Paulina.

 

Naye Robert Sengo (46) kutoka mkoani Geita anasema tangu Alhamisi yupo eneo hilo la Ukara na kwa bahati mbaya hajafanikiwa kumpata mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Buisya.

 

"Nimekesha nje tangu Alhamisi na mimi sina shida na kukesha kwenye baridi, nikiupata mwili wa mwanangu, nitashukuru kusudi nikampumzishe," anasema Sengo.

 

Tangu Alhamisi kivuko cha Mv Nyerere kilipozama, idadi ya watu imeendelea kuongezeka katika kisiwa hiki cha Ukara, wakifika kutambua miili na kuondoka nayo name viongozi kutoa pole.

 

Hii imesababisha uhaba wa vyumba vya kulala wageni. MCL Digital imefanya uchunguzi na kubaini kwamba, hakuna chumba hata kimoja kwa ajili ya wageni na wamiliki wa vyumba hivyo walianza kuchukua fedha taslimu tangu ya Alhamisi jioni.

 

Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Isaack Kamwelwe hadi kufikia jana (Septemba 22, 2018) jioni, takriban miili 171 ilikuwa imetambuliwa huku ilioopolewa ikiwa 218.