Wakili Mwale, wenzake wasomewa mashtaka 59

Muktasari:

  • Wakili Median Mwale na wenzake wamekua mahabusu kwa zaidi ya miaka mitano wakikabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha haramu jambo ambalo ni kosa kisheria na leo Septemba 24, 2018 wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka 59.

Arusha. Watuhumiwa watatu akiwemo wakili maarufu mkoani Arusha, Median Mwale wamesomewa mashtaka 59 pamoja na maelezo ya awali katika kesi ya kula njama kufanya kosa, utakatishaji fedha haramu na kughushi nyaraka kwa lengo la kujipatia fedha kinyume cha sheria.

Kesi hiyo iliahirishwa wiki iliyopita baada ya Wakili Median Mwale kudai asingeweza kuendelea kusikiliza maelezo yaliyokua yakitolewa mahakamani baada ya hali yake ya kiafya kubadilika ghafla na Jaji Issa Maige kukubali maombi yake.

Mawakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya, Hashim Ngole na Pius Hilla walipokezana kuwasomea mashtaka hayo ambayo watuhumiwa hao waliyakana kisha kusomewa maelezo ya awali ambayo pia nayo waliyakana.

Watuhumiwa wengine katika shauri hilo ni Boniface Mwimbwa aliyekua Meneja wa CRDB tawi la Meru na Elias Ndejembi aliyekua ofisa mwandamizi ambao pamoja na makosa mengine wanadaiwa kuidhinisha malipo kwa kutumia nyaraka zilizoghushiwa huku wakijua ni makosa kisheria.

Aliyekua mshitakiwa wa pili ambaye ni raia wa Kenya, Don Bosco Gichana alikiri makosa yake ya kula njama na kutakatisha fedha haramu kiasi cha dola za Marekani milioni 5,296,327.25 na kuamriwa kulipa faini au kutumikia kifungo gerezani.

Baada ya maelezo hayo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Issa Maige alitoa amri ya kuahirisha kesi hiyo hadi wakati mwingine utakaopangwa na Msajili wa Mahakama hiyo.

Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekomya amedai Mwale alitumia vitambulisho vya mkazi, barua kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hati za kusafiria na hundi bandia za benki ya Marekani kuhamisha fedha kwa watu mbalimbali.

Ameongeza miongoni mwa fedha alizojipatia kwa njia hiyo pia alinunua magari ya kifahari, nyumba na viwanja maeneo mbalimbali mkoani Arusha.

Katika hatua nyingine, Tibabyekomya amesema mashahidi na vielelezo katika shauri hilo vipo tayari kama vilivyoorodheshwa katika barua iliyowasilishwa mahakamani hapo Novemba 2017.

Hata hivyo, mawakili wa washitakiwa ambao ni Omari Omari, Emmanuel Mvula na Innocent Mwanga hawakuwa tayari kutaja idadi ya mashahidi na vielelezo kwa madai watafanya hivyo wakati utakapofika.