Wakili ataka Mbowe, Matiko wakamatwe, wafutiwe dhamana

Muktasari:

Kesi inayowakabili vigogo wa Chadema akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe imeendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku upande wa mashtaka ukitaka mtuhumiwa namba moja, Mbowe na Esther Matiko wafutiwe dhamana

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya viongozi wa Chadema, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam iamuru mshtakiwa wa kwanza, Freeman Mbowe na wa tano Esther Matiko wakamatwe.

Maombi hayo yametolewa leo Alhamisi Novemba 8, 2018 na wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, baada ya washtakiwa hao kushindwa kufika mahakamani.

Wakili Nchimbi amesema sababu za wadhamini wa washtakiwa hao kutofika mahakamani hazina msingi wowote na kwamba kwa maana hiyo ni sawa na washtakiwa wameruka dhamana.

Amesema vielelezo alivyowasilisha mdhamini wa Matiko ambaye ni mbunge wa Tarime Mjini, havina mashiko kwa sababu ni barua tu ya Katibu wa Bunge kumruhusu kusafiri.

Wakili Nchimbi amesema washtakiwa hao wako nje kwa dhamana na masharti maalum na kwamba kwa kuwa Bunge na Mahakama ni mihimili tofauti, basi barua hiyo ya Katibu wa Bunge haiwezi kuwa sababu ya kutohudhuria kesi yake.

Wakili Nchimbi ameiomba mahakama iamuru washtakiwa hao wakamatwe na wafikishwe mahakamani wajieleze ni kwa nini wasifutiwe dhamana.

Hata hivyo, Wakili John Mallya kwa niaba ya Wakili Peter Kibatala anayewatetea washtakiwa amepinga maombi hayo pamoja na mambo mengine akisema vifungu vya sheria alivyovitumia Wakili Nchimbi katika maombi hayo havihusiani na kile anachokiomba.

Pia amesema washtakiwa hao ni wabunge na hivyo hawawezi kuchukuliwa kama watu wa kawaida huku akisisitiza wadhamini wamewasilisha mahakamani hapo vielelezo kuthibitisha safari zao.

Hata hivyo, Wakili Nchimbi amesisitiza vifungu alivyotumia ni sahihi kwa kile alichokiomba kwani vinaelekeza mshtakiwa akiruka dhamana mahakama inatoa amri ya kuwakamata na kwamba mdhamini wa Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema maelezo aliyoyatoa ameidanganya Mahakama.

 

Mbowe anadaiwa amekwenda kutibiwa nje ya nchi, jambo ambalo pia limeibua utata wa nchi alikokwenda kutibiwa kwa kuwa taarifa za awali kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, alidaiwa kwenda kutibiwa Afrika Kusini lakini leo mdhamini wake amedai amekwenda kutibiwa Dubai.

Mdhamini huyo alipoulizwa na Hakimu Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo kuhusu taarifa za kutibiwa Afrika Kusini, alikana kuwa yeye hakusema hivyo.

Hakimu Mashauri alipombana kuwa kwa hiyo mara ya kwanza alitaja kuwa mshtakiwa amekwenda kutibiwa nchi gani, alisema yeye alieleza tu kuwa alisafirishwa kwenda kutibiwa nje ya nchi na alikuwa hajajua ni nchi gani na kwamba jana ndio alithibitisha ni Dubai.

Alipotakiwa kutoa vielelezo kuwa mshtakiwa huyo amekwenda kutibiwa hakuwa navyo na badala yake amesema mshtakiwa mwenyewe atakuja kuvitoa akirudi.

Kwa upande wa Matiko, mdhamini wake ameieleza Mahakama kuwa mshitakiwa huyo amesafiri kwenda Burundi kikazi, huku akiwasilisha mahakamani barua ya kutoka kwa Katibu wa Bunge ikimruhusu mshtakiwa huyo pamoja na nakala ya tiketi ya ndege.

Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja hizo sasa anaandaa uamuzi.

Endelea kufuatilia Mwananchi