Wakili azidiwa mahakamani, kesi yaahirishwa

Muktasari:

Kesi ya utakatishaji fedha haramu inayowakabili watuhumiwa wanne akiwemo wakili maarufu,  Median Mwale imeahirishwa hadi Septemba 24, 2018 baada ya afya ya Mwale kubadilika ghafla na kuiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo

Arusha. Kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili watuhumiwa wanne akiwemo wakili maarufu,  Median Mwale imeahirishwa hadi Septemba 24, 2018 baada ya afya ya Mwale kubadilika ghafla akiwa mahakamani.

 

Watuhumiwa wengine katika shauri hilo ni Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi huku raia wa Kenya, Don Bosco Gichana ambaye alikuwa miongoni mwao akiwa magereza baada ya kukiri kosa la kula njama na kutakatisha fedha haramu kiasi cha dola za Marekani milioni 5,296,327.25.

 

Kesi hiyo inayosikilizwa leo Septemba 21,2018 na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Issa Maige baada ya kuahirisha kesi hiyo kwa takribani dakika 30 kwa ajili ya mashauriano, alikubali maombi hayo na kuiahirisha hadi Septemba 24.

 

Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekomya akisaidiwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Martenus Marandu na Azael Mwatemi waliiomba mahakama kusikilizwa kwa maelezo ya awali baada ya mazungumzo yaliyokua yanaendelea ya kuendelea na kesi hiyo kati ya pande mbili,  kutokukamilika.

 

Hata hivyo, mawakili wa mshtakiwa wa kwanza, Omari Idd Omari na Emmanuel Mvula wamesema kutokana na muda wa mashauriano waliokuwanao kuwa mfupi hadi leo walikua hawajakamilisha mazungumzo yao.

 

"Ni kweli Jaji tumekua kwenye mazungumzo tangu kesi hii ilipoahirishwa mara ya mwisho lakini muda umekua mfupi na changamoto imekua upande wa mashtaka,” amesema.

 

“Kila mara unatakiwa kushauriana na ofisi ya Mwendesha Mashtaka naomba jambo hili liwe kwenye kumbukumbu za mahakama ili tuendelee na hatua inayofuata tukikubaliana tutaijulisha mahakama.”

 

Jaji Maige alikubaliana na maelezo ya mawakili hao na kutaka washtakiwa wakumbushwe mashtaka yanayowakabili kabla ya kusomewa,  ndipo Mwale alimwomba Jaji kesi iahirishwe kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

 

Mwale alimwonesha Jaji Maige dawa anazotumia baada ya kuulizwa ugonjwa huo umeanza lini,  na kujibu kuwa alianza kuugua  muda mrefu ila tangu alipofika mahakamani asubuhi alikuwa hajisikii vizuri.

 

Kufuatia hatua hiyo, wakili Tibabyekomya amesema hakuwa na  pingamizi na kesi kuahirisha.

 

Mshitakiwa huyo na wenzake walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti  kati ya mwaka 2009 na 2012.