Kampuni ya Six Telecoms, vigogo wake kizimbani

Muktasari:

Wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya dola 3.748 milioni za Marekani (sawa na Sh8 bilioni). 

Dar es Salaam. Kampuni ya Six Telecoms Limited na vigogo wake wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi likiwemo la kusababisha hasara ya dola 3.748 milioni za Marekani (sawa na Sh8 bilioni).

Wakili wa Serikali, Jehovaness Zacharia  amewasomea mashtaka washtakiwa leo Jumatatu, Novemba 20,2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Mbali ya kampuni hiyo, wengine waliosomewa mashtaka na vyeo vyao kwenye mabano ni Hafidhi Shamte maarufu Rashidi  Shamte (mhandisi na mkurugenzi mkuu) Peter Noni (mfanyabiashara na mkurugenzi), Ringo Tenga (mwanasheria na mkurugenzi) na Noel Chacha (mkuu wa fedha).

Katika kesi hiyo namba 73 ya 2017, wakili Zacharias amedai kati ya Januari Mosi, 2014 na Januari 14,2016  walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha dola 0.25 za Marekani kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, wanadaiwa kwa udanganyifu na kwa nia ya kuepuka malipo, walishindwa kulipa dola 3,282,741.12 kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama malipo ya mapato.

Katika shtaka lingine, wanadaiwa kushindwa kulipa ada za udhibiti za dola 466,010.07 kwa TCRA na pia, wanadaiwa

walijipatia, walitumia au walisimamia dola 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana mashtaka yaliyotangulia.

Kampuni ya Six Telecoms Limited inadaiwa ilijipatia, ilitumia na kusimamia dola 3,282,741.12 wakati ikijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu yanayotokana mashtaka yaliyotangulia.

Kwa pamoja washtakiwa wanadaiwa waliisababishia TCRA hasara ya dola 3,748,751.22 (sawa na Sh8 bilioni).

Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.

Washtakiwa wanatetewa na mawakili Dk Masumbuko Lamwai, Dk Wilbert Kapinga na Grayson Shayo.

Dk Lamwai aliomba Mahakama iyaondoe mashtaka hayo kwa sababu yana upungufu; hayaelezi nani kafanya nini na kwa upande wa kosa la utakatishaji wa fedha haliendani na shtaka husika.

Wakili Jehovaness alidai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi na kama wanataka kupinga waende Mahakama Kuu.

Alidai upelelezi haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Novemba 24 na washtakiwa wamepelekwa rumande.