Wakili wa Serikali aomba kesi ya mbunge wa Chadema ifutwe

Mbunge wa Bukoba Mjini(Chadema),Wilfred Lwakatare

Muktasari:

  •  Ni kesi ya Lwakatare ilikuwa ikimuhususha na njama za kumdhuru aliyekuwa mhariri wa Mwananchi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), ambaye kwa sasa ni  Mbunge wa Bukoba Mjini(Chadema),  Wilfred Lwakatare na mwenzake, Ludovick Rwezaura.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amewaachia huru washtakiwa hao leo Alhamisi mara baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuomba kesi hiyo ifutwe chini ya kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofabnyiwa marekebisho 2002 na Mahakama kuridhia.

Kishenyi aliomba kesi hiyo ifutwe chini ya kifungu hicho kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo hakimu aliwaachia huru washtakiwa hao leo saa 4 asubuhi.

Wakati kesi hiyo ikiondolewa mahakamani hapo alikuwapo Lwakatare  pekee na mwenzake hakufika kutokana na kuwa matatizo ya kifamilia.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Machi 20, 2013.

Katika kesi hiyo walikuwa wakidaiwa kuwa Desemba 28, 2013  katika eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja walikula njama za kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.

Baada ya kuachiwa huru, Lwakatare alimshukuru Mungu kwa kuwa na siku njema na yenye furaha kwake.