Wakili wa kina Kitilya ataka kujua upelelezi umefikia wapi

Muktasari:

Washtakiwa hao wanadaiwa kughushi nyaraka za makubaliano Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic, Dar es Salaam.

Dar es Salaam.Wakili Majura Magafu ameutaka upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), Harry Msamire Kitilya na waliokuwa maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon kueleza upelelezi umefikia wapi.

Magafu ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 28 saa 3:30 asubuhi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri mara baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kueleza kuwa kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kwa hatua ya upelelezi leo (jana) ana udhuru.

Hivyo aliomba mahakama itoe tarehe nyingine na baada ya kusomewa maelezo hayo, Wakili Magafu alidai mbali na shauri lililopo kwa Hakimu Mkeha, wanahitaji kujua upelelezi umefikia hatua gani.

Magafu alibainisha kuwa mara ya mwisho upande wa mashtaka ulieleza kuna nyaraka wanasubiri kutoka nje ya nchi na kwamba leo (jana) wangeweza kueleza hali halisi ya upelelezi.

Kesi imeahirishwa hadi Agosti, 11, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Kitilya na wenzake wakati wakitoka mahabusu kwenda mahakamani kusikiliza kesi hiyo walionekana wakitabasamu na kusalimiana na ndugu zao. 

Awamu ya kwanza ya vielelezo hivyo kutoka Uingereza vimeshapokelewa. Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Agosti 2, 2012, Sinare kwenye Makao Makuu ya Benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni kwa nia ya kudanganya aliandaa nyaraka ya pendekezo akijaribu kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya Uingireza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania watatoa mkopo wa Dola za Kimarekani 550milioni kwa Serikali  ya Tanzania kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.

Inadaiwa kuwa Agosti 2, 2012, Sinare alitoa nyaraka za uongo za mapendekezo ya kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya Uingereza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo wa Dola za Kimarekani 550milioni na kuziwasilisha katika ofisi za Wizara ya Fedha wakati akijua kuwa si kweli.

Aliendelea kudaiwa kuwa Septemba 20, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic yaliyopo Kinondoni, alitenda kosa la kughushi barua.

Sinare anadaiwa kughushi barua ya mapendekezo ikionyesha kuwa Benki ya Standard ya Uingereza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania watatoa mkopo wa Dola 550milioni kwa Serikali ya Tanzania kama ada ya uwezeshaji wa asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.

Agosti 21, 2012, Sinare anadaiwa kuwa kwa lengo la kulaghai aliwasilisha nyaraka hizo za uongo kuiwezesha Serikali ya Tanzania kupata mkopo huo wa kiasi hicho cha ada ya uwezeshaji, katika ofisi za Wizara ya Fedha.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi nyaraka za makubaliano kwamba Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic makao makuu Kinondoni Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walighushi waraka wa makubaliano wa Novemba 5, 2012.

Inadaiwa kuwa waraka huo ulikusudia kuonyesha kuwa Stanbic Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (Egma) Limited kuwezesha upatikanaji wa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa ajili Serikali ya Tanzania.

Wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani 6 milioni, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Kati ya Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na Kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.