Saturday, October 28, 2017

Wakulima, wafugaji warushiana maneno mbele ya Waziri Ulega

 

By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Tanga. Wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Perani wilayani Mkinga wametupiana maneno mbele ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa kinara wa kuvamia eneo kwa shughuli mbalimbali.

Tukio hilo lilitokea jana wakati Ulega alipotembelea kijiji hicho kwa lengo la kukutana na wakazi wa eneo hilo wakiwamo wakulima na wafugaji kwa ajili ya kuzungumza changamoto zinazowakabili.

Wakulima walimweleza Ulega kuwa wamekuwa wakitumia muda mwingi kulinda mashamba yao kutokana na uwapo wa kundi kubwa la ng’ombe wanaopelekwa na wafugaji.

“Mheshimiwa waziri huwezi kufanya chochote kama umepanda mazao shambani kwa jinsi ng’ombe wanavyoshambulia shamba lako. Ni vigumu shamba kufuata ng’ombe sasa nawashangaa wenzetu wanavyosema tunawavamia,” alisema Said Kokoi.

Alisema hali inakuwa ngumu inapotokea mkulima anajaribu kuwaondoa ng’ombe hao shambani kwake kwa kuwa kundi la wafugaji wa jamii ya wamasai linamfuata na kuanza kumshambulia kwa silaha.

“Jambo hili linatuuma mheshimiwa kwa sababu watu wanapotea katika mazingira ya kutatanisha na siku ya kuonekana wanakuwa maiti,” alisema Kokoi.

Hata hivyo, mfugaji Moi Sangaine alimweleza Ulega kuwa wakulima wamekuwa wakorofi kwa kuziba njia ambayo mifugo yao inatakiwa ikanywe maji.

“Wakulima wanaziba njia za mifugo yetu kwenda kunywa maji kutokana na kilimo chao. Ukithubutu kupitisha mifugo ni mgogoro kwa sababu unaharibu mazao yao,” alisema Sangaine.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Letinga Oyaya alisema eneo hilo lina mpango wa matumizi bora ya ardhi lakini anashangaa ni kwa nini mamlaka husika zinashindwa kusimamia jambo hilo na hivyo kusababisha mgogoro.

“Endapo mpango huu ungekuwa unatekelezwa kikamilifu hatuwezi kufikia hatua hii ya mapigano na kusababisha watu kuishi kwa hofu. Nimeliwasilisha jambo hili mara nyingi katika wilaya lakini hakuna utekelezaji,” alisema Oyaya.

Kutokana na malalamiko hayo, Ulega aliwasihi wafugaji na wakulima kuacha mapigano.

Ulega alisema huu ni wakati wa kuishi kwa amani na utulivu kwa kuwa suala hilo litafikishwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.

Pia, aliwatoa hofu wafugaji kuhusu mchakato wa upigaji chapa wa ng’ombe na kusema Serikali haina nia ya kuchukua mifugo bali utaratibu huo umelenga kutambua mifugo yote nchini.

-->