Wakulima ‘walizwa’ pembejeo

Muktasari:

Usambazaji wa pembejeo za wakulima mara kadhaa umekuwa ukikumbwa na changamoto nyingi ikiwamo mawakala wasio waaminifu ambao huuza kwa bei ya juu au kuwapatia wakulima zisizo na ubora.

Shinyanga. Wakulima zaidi ya 200 wa kata ya Salawe katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa wamepelekewa orodha ya majina yao yaliyosainiwa na kiwango cha fedha kwa kila mmoja bila wao wenyewe kufahamu aliyeyaandika na kusaini, huku ikionyesha wameshachukua pembejeo kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo.

Akizungumza mjini hapa juzi, Mwenyekiti wa wachukuaji pembejeo hizo, Shija Makingi alisema alishtukizwa na hatua ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumhoji kama amehusika kwenye uchukuaji wa pembejeo za wakulima hao.

“Wala sijui lini niliwasainisha wakulima, hata wao hawafahamu ningekuwa nimehusika wangefahamu, yaani nimeshangaa kukuta jina langu pia limeorodheshwa kama mwenyekiti na kusaini vocha ya Sh75,000,” alisema Makingi.

Baadhi ya wakulima ambao majina yao yamesainiwa vocha huku wakiwa wametofautiana kiwango cha fedha walisema wameshtushwa kuona wanaitwa mmoja mmoja kuhojiwa na maofisa wa Takukuru na kukana kujua lolote kuhusiana na suala hilo.

Wakulima hao, Daudi Mbungu, Zacharia Msalaba, John Shinja, John Shikombe na James Lyochi walikana kuchukua wala kujua chochote kuhusiana na pembejeo hizo na kueleza kushtushwa kwao na jambo hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele, Majaliwa Mikilo alisema licha ya majina ya wachukua pembejeo kupelekwa ofisi ya mtendaji wa kijiji wakidaiwa kuchukua vocha hizo, lakini walipoulizwa walikana kufanya hivyo.

Naye Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu alisema ameshangazwa kuona wakulima wakihojiwa bila yeye kufahamu ni lini walisaini vocha hizo, kampuni gani iliyohusika au watu waliofanya kitendo hicho alichokieleza kuwa ni utapeli dhidi ya wakulima.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Edward Maduhu alisema yeye hafahamu kitu chochote kwani taarifa hizo bado hazijamfikia.

Kwa upande wake, Kamanda wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Gastor Mkono alisema tukio hilo ni la kweli ila hawezi kuzungumza chochote kuhusiana na hatua wanazochukua na hatua waliyofikia katika uchunguzi wanaoufanya akisema hadi hapo utakapokamilika atatoa taarifa.

Jitihada za Mwananchi kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Simon Haule aweze kueleza kama kuna mtu yeyote anashikiliwa au anatafutwa kutokana na suala hilo hazikufanikiwa kutokana na simu yake ya mkononi kutopatikana hewani.

Aidha, alipotafutwa mkuu wa wilaya hiyo, Jusintha Mboneko ili kujua kama ana taarifa zozote juu ya suala hilo na mambo mengine yanayohusiana nae simu yake ya mkononi haikupatikana hewani.