Tuesday, October 25, 2016

Wakulima Mkonge waanza safari, waomba pembejeo za ruzuku

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi rsaid@mwananchi.co.tz

Korogwe. Katika kuhakikisha wanajikomboa, wakulima wa mkonge wameshauriwa kununua hisa kwenye viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuondokana na kuendelea kuzalisha malighafi pekee.

Mkoa wa Tanga mwaka 1964 ulifikia uzalishaji wa asilimia 65 ya tani 234,000 za mkonge zilizozalishwa nchini.

Uzalishaji wa mkonge uliendeshwa katika mashamba makubwa ambayo yalikuwa na eneo la wastani wa hekta 3,000, huku asilimia 75 yakimilikiwa na wageni kutoka nje.

Mkonge uliingizwa nchini kwa magendo kutoka nchini Mexico mwaka 1893 na Mtafiti wa Mimea na Udongo wa Kijerumani, Dk Richard Hindorff. Inaelezwa kuwa alichukua miche 1,000 kutoka Jimbo la Yucatan, Mexico ambako ndiko asili ya jina Katani.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa Kiwanda cha Kusindika Mkonge katika Shamba la Magoma wilayani Korogwe juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte alisema iwapo watapigania kuwa na hisa viwandani, itawasaidia kujua kinachoendelea sokoni.

Shamte alisema kilimo bila ya viwanda siyo endelevu na kwamba, kitakuwa ni kuganga njaa.

“Tanzania ya viwanda lazima ianzie katika viwanda ambavyo vitabadilisha mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge wa Shamba la Magoma, Omar Athuman alisema wanaomba kupewa hati miliki ya mashamba wanayotumia ili wawe na uhakika wa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.

Athuman alisema wanashindwa kukopa kutokana na kukosa hatimiliki za mashamba.

Pia, alisema wakulima wanaomba ruzuku kama wenzao wa mazao mengine kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella aliipongeza Kampuni ya Katani Limited kwa uamuzi wa kuinua na kuendeleza kilimo cha mkonge.

Shigella aliwaeleza kuwa wakulima wa katani ni wajasiriamali na wawekezaji wa kweli ambao kwa pamoja wanatekeleza kwa vitendo vita dhidi ya umasikini, hivyo kutengeneza ajira na mzunguko wa fedha katika eneo hilo.

-->