Wakulima jela kwa ujangili

Muktasari:

Washtakiwa hao Gidamis Giyamu (31) na Petro Kilo Kinangai (31), wote wakulima na wakazi wa Mdori, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, wamehukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia na kushindwa kulipa faini ya mamilioni iliyokuwa mbadala.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Karatu, imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela wakazi wawili wa wilayani Babati, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyara za Serikali katika kesi mbili tofauti.

Washtakiwa hao Gidamis Giyamu (31) na Petro Kilo Kinangai (31), wote wakulima na wakazi wa Mdori, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, wamehukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia na kushindwa kulipa faini ya mamilioni iliyokuwa mbadala.

 Katika kesi ya kwanza, Mahakama hiyo imemhukumu kifungo hicho Giyamu baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh600,791,500 na Kinangai baada ya kushindwa kulipa Sh290,172,000.

Hukumu za kesi hizo zote zilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ally Mkama aliyekuwa akisikiliza kesi hizo zote wiki iliyopita.