Wednesday, May 16, 2018

Wakulima kuondolewa mzigo wa ada na tozo 21

Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba akizungumza

Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba akizungumza bungeni alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Wizara ya Kilimo imependekeza kufutwa ada na tozo 21 katika mazao, uzalishaji wa mbegu na vyama vya ushirika.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo jana, Waziri Charles Tizeba alisema ada na tozo zinazopendekezwa kufutwa zimeonekana kuwa kero kwa maendeleo ya sekta ya kilimo.

Dk Tizeba alitoa mchanganuo wa ada na tozo zinazopendekezwa kufutwa akisema katika zao la chai ni tatu, kahawa (3), tumbaku (2) na tozo moja kwa sukari na moja pamba.

“Kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, inapendekezwa kufutwa tozo tano kwenye uzalishaji wa mbegu,” alisema.

Dk Tizeba alisema kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya ushirika nchini, inapendekezwa tozo sita katika ngazi za ushirika zifutwe.

Alisema wizara itaendelea kuchambua na kubaini ada na tozo ambazo bado ni kero kwa wakulima nchini na kuzifuta.

“Lengo ni kubakiza ada na tozo ambazo zina mahusiano ya moja kwa moja na uendelezaji wa mazao husika, kama vile uendelezaji wa utafiti wa mazao,” alisema.

Dk Tizeba alisema wamewasilisha Wizara ya Fedha na Mipango mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kodi na tozo kwa lengo la kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji na uendeshaji biashara katika shughuli za kilimo.

“Mapendekezo hayo yanalenga kutoa unafuu wa kodi katika vifungashio vya mazao na mbegu za mazao ya kilimo, mabomba ya kunyunyuzia dawa, mashine na mitambo ya usindikaji wa mazao, miundombinu ya uzalishaji na hifadhi ya mazao ya bustani na kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani usio sawa na bidhaa kutoka nje ya nchi,” alisema.

Alisisitiza kuwa mpango wa wizara ni kuhakikisha kero zote zinazokwamisha maendeleo ya mazao ya kilimo zinashughulikiwa.

Tozo 80 zilifutwa 2017

Katika bajeti ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka jana, Serikali ilifuta kodi, ada na tozo 80 kati ya 139 za mazao ya kilimo ambazo ni kero kwa wakulima, huku ikipunguza viwango vya tozo vinne ambavyo vimeonekana kuwa ni kero.

Dk Tizeba alisema katika zao la tumbaku tozo 10 zitafutwa na mbili zitapunguzwa viwango, katika kahawa 17 zilifutwa na tozo moja itapunguzwa viwango.

“Tasnia ya sukari tozo 16 zitakafutwa. Katika pamba ni kodi mbili na tasnia ya korosho zitakazofutwa ni mbili na tozo moja iliyokuwa kero itafutwa katika tasnia ya chai,” alisema.

Dk Tizeba alisema wamefuta tozo tatu kwenye mbolea na moja itapungua kiwango.

“Tozo saba zilizokuwa kwenye mbegu zimefutwa na tozo pekee iliyokuwa katika Mfuko wa Pembejeo ya Ada ya Nyaraka nayo imeondolewa,” alisema.

Pia waziri huyo alisema katika kuimarisha ushirika nchini, Serikali itafuta tozo 20 zilizokuwa kwenye ushirika katika ngazi mbalimbali.

Changamoto za ushirika

Dk Tizeba alisema ushirika bado unakabiliwa na changamoto ikiwemo ubadhirifu wa mali za vyama vya ushirika unaofanywa na watendaji wa vyama wasio waaminifu.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni uelewa mdogo juu ya haki, wajibu na majukumu yao kama wamiliki wa vyama.

“Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inaimarisha usimamizi kwa kuongeza kasi ya ukaguzi wa vyama, kuwajengea uwezo viongozi na kutoa mafunzo kwa wanachama kuhusu haki na wajibu wao,” alisema.

Dk Tizeba alisema Serikali imeendelea kufuatilia ili kuzirudisha mali za vyama vya ushirika zilizoporwa na watu binafsi au taasisi pamoja na kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika wa ubadhirifu.

Alisema viongozi 57 na watendaji wa vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) walihojiwa na kuandaliwa hati za madai kwa tuhuma za kufanya ubadhirifu wa Sh5.95 bilioni.

Waziri huyo alisema katika kuimarisha usimamizi wa Saccos, wizara hiyo imeingia makubaliano na taasisi ya Dun and Bradstreet Credit Bureau Tanzania Ltd ya kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa usimamizi ambao sasa upo kwenye majaribio.

Dk Tizeba alisema mfumo huo utawezesha kupatikana taarifa za mara kwa mara juu ya maendeleo ya Saccos na kufanya usimamizi kwa ufanisi na urahisi zaidi.

Uzalishaji sukari wapungua

Dk Tizeba alisema uzalishaji wa sukari kwa msimu wa mwaka 2017/18 umeshuka ukilinganishwa na msimu wa mwaka 2016/17 kutokana na ukosefu wa mvua za kutosha mwanzoni mwa msimu.

Alisema suala hilo lilitokana na hali ya hewa iliyoathiri ukuaji wa miwa na kusababisha kudumaa kwa zao hilo, hasa kwa wakulima wadogo na kusababisha kiwango cha sukari kupungua.

Kuhusu ununuzi wa nafaka nchini, Dk Tizeba alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umepanga kununua tani 28,200 za nafaka kupitia vituo vya ununuzi, vikundi na vyama vya wakulima.

-->