Wakulima wa mkonge kunufaika

Muktasari:

Bodi ya Mkonge nchini (TSB), imesema itayafanyia kazi maagizo ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba ya kusimamia mchakato wa upandishaji wa malipo ya vibarua

Bodi ya Mkonge nchini (TSB), imesema itayafanyia kazi maagizo ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba ya kusimamia mchakato wa upandishaji wa malipo ya vibarua wanaofanya kazi kwenye mashamba ya Mkonge kwa kuitisha vikao vya vya vyombo vinavyohusika.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkurugenzi wa TSB,Yunus Msika ametoa ahadi hiyo leo Novemba19 alipokuwa akizungumza na Mwananchi iliyotaka kujua ni lini agizo la Waziri Tizeba la kuongeza mishahara ya vibarua wanaofanya kazi kwenye mashamba ya Mkonge litafanyiwa kazi?

Waziri Tizeba ametoa  agizo hilo alipotembelea shamba la Mkonge la Kwaraguru SFI Tanzania lililopo Wilayani hapa ambapo alizungumza na wakulima na wakata mkonge aliowakuta shambani hapo waliomweleza kwamba wamekuwa wakilipwa kati ya Sh 150,000 na 120,000 kwa mwezi.

 

Akiwa shambani hapo wakulima hao walimweleza Waziri Tizeba kuwa ingawa baadhi yao wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 shambani hapo lakini ajira zao ni mkataba wa miezi sita na ikiisha wanaandikishwa upya.

 

Wamesema kutokana na mkataba huo wengi wao wamekuwa wakilipwa mshahara wa kati ya sh 120,000 na  Sh 150,000 na kuomba waongezwe kwa kuwa hautoshelezi mahitaji.

 

"Nakuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge fanyia kazi suala hili,haiwezekani wafanyakazi hawa wengine ni wazee kulipwa kiasi

 hiki...ni kidoto mno wanafanya kazi ngumu hapa shambani"amesema

Tizeba.

 

Meneja Mkuu wa SIF Tanzania Ltd, Thys Greeff aliifahamisha Mwananchi kuwa kiwango cha malipo kwa wafanyakazi wote  wa mashamba ya mkongewakiwamo vibarua huwekwa na Idara ya kazi,chama cha wafanyakazi wa mashambani (TPAW),Chama cha wakulima wa Mkonge (SAT).

 

"Sisi tunalipa baada ya Serikali kupitia idara yake ya kazi kwa kushirikiana na SAT, TPAW kukaa na kupanga viwango vya mishahara,na hii inawezekana kuna vigezo ambavyo vyombo hivyo huangalia kabla ya kutuletea sisi kwa utekelezaji"amesema Greeff

 

Mwenyekiti wa (SAT),Deogratius Ruhinda alisema kuna taratibu za kufuatwa kabla ya kuweka viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wa mashamba ya mkonge ikiwamo kuangalia gharama za uendeshaji na faida itokanayo na biashara hiyo.

 

‘’Nitaanza kukaa na vyombo vinavyohusika na upangaji wa mishahara kwa wafanyakazi wa kwenye mashamba ya mkonge ili kuanza mchakato wa kupandisha viwango kama alivyoagiza Waziri"amesema Msika