Wakulima wageukia mkaa

Muktasari:

  • Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili maeneo ya wilaya za Kwimba na Magu katika vijiji tofauti unaonyesha kuwa, msimu wa kilimo unaoanza Septemba hadi Desemba hakukuwa na mvua za kutosha hali iliyosababisha mazao kukauka.
  • Hali hiyo iliwalazimisha wananchi hao kugeukia biashara ya mkaa ili mkono uende kinywani.

Mwanza. Kutokana na kuchelewa kwa mvua za masika kwa maeneo mengi nchini, baadhi ya wakulima hasa wa vijijini wageukia biashara ya kuchoma na kuuza mkaa ili kujipatia kipato kwa ajili ya kutunza familia.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili maeneo ya wilaya za Kwimba na Magu katika vijiji tofauti unaonyesha kuwa, msimu wa kilimo unaoanza Septemba hadi Desemba hakukuwa na mvua za kutosha hali iliyosababisha mazao kukauka.

Hali hiyo iliwalazimisha wananchi hao kugeukia biashara ya mkaa ili mkono uende kinywani.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wauzaji wa mkaa wilayani Magu, Kisendi Kushosha alisema hawakuwa na kazi ya kuwaingizia kipato.

Mkulima mwingine, Nestory Shija alisema wanachokifanya ni kukata miti wanayoona imekomaa au kuchimba visiki kisha kuchoma mkaa.

Januari 6, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiwa ziarani Kwimba, alipokewa na zaidi ya wakazi 300 wa Kata ya Mwagi wakiwa na mabua ya mahindi mikononi wakionyesha namna zao hilo lilivyoathiriwa na ukame.