Wakulima walilia kiwanda cha kusindika

Muktasari:

  • Wakulima hao ambao muda mrefu wamekuwa wakizalisha matikiti maji wamesema kuwa ingawa wanatumia gharama kubwa za kilimo hicho, lakini hawana soko la uhakika la zao hilo jambo ambalo limekuwa likiwalazimu kuyauza kwa mkopo kwa madalali huku mengine wakiyauza kwa rejareja mitaani na sokoni

Wakati Serikali ikiendelea kusisitiza  suala la uwekezaji  hususan  katika ujenzi wa viwanda nchini ili  kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020 kwa kuzalisha na kuuza bidhaa mbalimbali zitokanazo na malighafi za ndani, wakulima wa matikiti maji wilayani Kibaha mkoani hapa  wameomba kiwanda cha kusindika zao hilo.

Wakulima hao ambao muda mrefu wamekuwa wakizalisha matikiti maji wamesema kuwa ingawa wanatumia gharama kubwa za kilimo hicho, lakini hawana soko la uhakika la zao hilo jambo ambalo limekuwa likiwalazimu kuyauza kwa mkopo kwa madalali huku mengine wakiyauza kwa rejareja mitaani na sokoni.

"Tunaiomba Serikali iangalie njia ya kutafuta wawekezaji wajenge kiwanda cha kukausha ama kusindika zao hili la matikiti maji ili tuwe tunawauzia  kwa wakati na kwa bei yenye maslahi," amesema Felician Bwemelo mkulima wa matikiti maji kutoka Mwendapole Kibaha.

Bwemelo amesema kwa sasa wanalazimika kuuza matikiti yao kwa madalali kwa njia ya mkopo na kwa bei ndogo.
"Hivi sasa tunauza ujazo wa lori lenye tani 10 kwa Sh2 milioni kutoka Sh4 milioni…hili suala linasikitisha sana, "amesema na kuongeza;

"Naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutusaidia sisi wakulima wa matikiti maji, tukipata kiwanda cha kusindika itakuwa afadhali kwa sababu tutakuwa na uhakika wa mauzo.”
Naye John Mwaluko amesema kuwa  inapofikia wakati wa mavuno madalali hao wamekuwa wakifika kwenye mashamba  yao na kufanya maelewano ya bei kisha kuvuna na  kuondoka na baada ya hapo hawarudi ili kufanya malipo.
Kwa upande wake Joshua Makani  amesema  kuwa wakati umefika kwa  Serikali kuangalia  uwezekano wa kujenga viwanda vya kusindika juisi  inayotokana na mazao hayo  ili wakulima waweze kuuza kiurahisi tofauti na ilivyo sasa.