Wakulima washauriwa kukopa

Muktasari:

  • Alitoa rai hiyo juzi, alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani katika Kijiji cha Matufa wilayani Babati, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara.
  • “Mkurugenzi wenu amesema hapa kuwa ni vigumu kwa wakulima kupata mikopo na inayotolewa na benki ina riba kubwa. Napenda niwasisitize kuwa msiogope kukopa kwa sababu hakuna tajiri duniani aliyeendelea bila kukopa,” alisema.

Babati. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakulima wakubwa na wadogo wa miwa kwenye Kiwanda cha Sukari cha Manyara wachukue mikopo kama wanataka kuendeleza kilimo hicho.

Alitoa rai hiyo juzi, alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani katika Kijiji cha Matufa wilayani Babati, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara.

“Mkurugenzi wenu amesema hapa kuwa ni vigumu kwa wakulima kupata mikopo na inayotolewa na benki ina riba kubwa. Napenda niwasisitize kuwa msiogope kukopa kwa sababu hakuna tajiri duniani aliyeendelea bila kukopa,” alisema.

Hata hivyo, aliwakumbusha wakulima hao kwamba wakishakopa, wasisahau kuwa dawa ya deni ni kulipa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema Majaliwa aliwaeleza kuwa zipo benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima ambazo ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), NMB, CRDB, Benki ya Kilimo (Tadb) na Benki yaTIB.

Aliwataka wakurugenzi wa kiwanda hicho waharakishe uagizwaji wa mitambo mipya ili kiongeze uzalishaji.

“Napenda niwahakikishie wakurugenzi kuwa Serikali imedhamiria kulinda viwanda vya ndani. Tunataka muongeze uzalishaji ili kufidia pengo lililopo. Tutaruhusu waagizaji walete sukari kutoka nje baada ya kujiridhisha kuwa uzalishaji wa ndani umejitosheleza,” alisema.

Alisema takwimu za mahitaji ya sukari nchini zinapaswa kupitiwa kwa sababu hazitoi picha halisi. “Tanzania ina watu milioni 50 lakini mahitaji ya sukari tunaambiwa ni tani 420,000 kwa mwaka. Wenzetu wa Kenya wako milioni 45 lakini mahitaji yao ni tani 800,000 kwa mwaka. Tulishawaambia wapitie upya hizi takwimu zao.”

Awali, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Ofisa Mahusiano wa kiwanda hicho, Dipak Odedra alisema kilianzishwa mwaka 2006 kikiwa na uwezo mdogo wa kusaga tani 50 za miwa kwa siku lakini sasa kina uwezo wa kusaga tani 500 kwa siku.

“Kuongezeka kwa uzalishaji na kukua kwa kiwanda kumechangiwa na mikataba ya kuwashirikisha wakulima wadogo, kuwakopesha mitaji tangu kutayarisha mashamba, kupanda mbegu, usafiri na utaalamu lengo likiwa kununua miwa yao inapokuwa tayari kuvunwa,” alisema.

Odedra alisema mpango huo shirikishi wa kupanda miwa unahusisha vijiji zaidi ya 10 na jumla ya eka 1,150 zinalimwa na wakulima wadogo waliohamasika na kuona faida za kilimo hicho.