Wakurugenzi kampuni nne waburuzwa mahakamani

Muktasari:

Wanatuhumiwa kutoshirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutoa taarifa za waajiriwa wao


Dar es Salaam. Wakurugenzi watendaji wa kampuni nne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Februari 19, 2018 wakikabiliwa na mashtaka ya kutojisajili na kupeleka taarifa muhimu za wafanyakazi katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Wakurugenzi hao ni Abshir Gure na Farhiya Wrsame wa kampuni ya Lasar Logistic, Joseph Alexander wa Kamanda Security Guards Ltd, Riziki Shemdoe na Deusdedit Kibassa wa ENCC Consultants na Malakhara Semis na Shafeek Purayil wa Kampuni ya Spash International.

Washtakiwa hao leo asubuhi waliingia katika ukumbi wa mahakama ya wazi namba moja na baada ya muda Hakimu Mfawidhi Victoria Nongwa aliingia na kesi zao zikaanza kuitwa kwa nyakati tofauti.

Washtakiwa hao wametimiza masharti ya dhamana na kesi zao zimeahirishwa hadi Februari 22, 2018 ambapo watasomewa maelezo ya awali.

Washtakiwa wanadaiwa kufanya makosa hayo kinyume cha kifungu cha 71 (1) (a) na 71 (4) cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi sura ya 263 iliyorejewa mwaka 2015.

Wanadaiwa kushindwa kutoa taarifa kwa ofisa wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi ambapo ni kinyume na kifungu cha 8 (5) (c) kikisomwa pamoja na kile cha 96 cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi sura ya 263.

Kwa pamoja washtakiwa hao wanatetewa na mawakili wanne akiwamo Jeremiah Mtobesya na Steven Mosha.

Akizungumza nje ya mahakama, Mwanasheria wa WCF, Deo Victor alisema kabla ya WCF kuchukua hatua ya kuwafikisha mahakamani, washtakiwa walipewa taarifa ya kutekeleza takwa hilo la kisheria katika tarehe mbalimbali kati ya Septemba 2017 hadi Januari 2018, lakini walishindwa.

Ameeleza kuwa washtakiwa hao endapo watapatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo kisichozidi miaka mitano au faini isiyozidi Sh50 milioni ama vyote kwa pamoja.

Amesema kupandishwa huko kizimbani kwa waajiri hao  ni mwanzo na kwamba, mfuko utachukua hatua kama hiyo kwenye mikoa yote Tanzania Bara na kuwaasa waajiri kutoka sekta za umma na binafsi upande wa Tanzania Bara.