Wakuu wa EAC kukutana kesho Dar

Muktasari:

Katika mkutano huo wa 18 Tanzania itakabidhi  nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa Uganda, baada ya kuishika kwa miaka miwili.

Dar es Salaam. Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajia kufanya mazungumzo ya pamoja katika  mkutano wa kawaida wa  18 utakaofanyika kesho (Jumamosi), Ikulu jijini hapa. 

Mkutano huo unatarajiwa kupokea  ripoti ya usuluhishi ya kamati inayoongozwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu mgogoro wa Burundi.

 Mambo mengine yatakayozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na taarifa na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa katika mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo.

 Masuala hayo ni pamoja na namna ya kuwezesha uundaji wa magari katika   Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupunguza uagizaji wa magari yaliyotumika kutoka nje ya Jumuiya, mapitio kuhusu sekta ya nguo na ngozi.

Masuala mengine ni pamoja na  kuzuia ama kuondoa uagizaji wa nguo na viatu vya mtumba kutoka nje.

Wakuu hao wa Nchi pia wanatarajia kujadili namna endelevu ya uchangiaji wa bajeti ya Jumuiya hiyo kwa nchi wananchama.