Wakwepa kodi ‘wamtia wazimu’ DC

Muktasari:

  • Katika robo ya kwanza ya mwaka, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilikusanya Sh1.9 bilioni zikiwa ni ushuru wa huduma, kati ya hizo Sh1.2 bilioni ni kutoka Mgodi wa North Mara Acacia na Sh700 milioni kwa makandarasi wanaofanya biashara na mgodi huo.

Tarime. Baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kukusanya Sh1.9 bilioni kwa robo ya kwanza ya mwaka, huku wafanyabiashara wa Halmashauri ya Mji wakidaiwa kukwepa kodi ya zaidi ya Sh120 milioni, mkuu wa wilaya hiyo, Glorious Luoga ameapa kuwadhibiti wakwepa kodi wote bila hofu wala kujali utajiri, umaarufu au wadhifa wa mtu.

Katika robo ya kwanza ya mwaka, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilikusanya Sh1.9 bilioni zikiwa ni ushuru wa huduma, kati ya hizo Sh1.2 bilioni ni kutoka Mgodi wa North Mara Acacia na Sh700 milioni kwa makandarasi wanaofanya biashara na mgodi huo.

Kwa kipindi hicho, Halmashauri ya Mji ilikusanya takriban Sh60 milioni kwa wafanyabiashara, huku ikidaiwa kupoteza zaidi ya Sh120 milioni.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Sh21 milioni kwa ajili ya mikopo kwa makundi ya vijana na wanawake wilayani hapa juzi, Luoga alisema katika maisha yake anamhofia Mungu anayempa uhai na Rais John Magufuli aliyemteua.

“Fedha hizi zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, bila watu kulipa kodi haziwezi kupatikana au zitakuwa kidogo. Lazima kila mtu alipe kodi stahiki kwa maendeleo yetu wote,” alisema Luoga.

Alisema amepata taarifa za baadhi ya viongozi wakiwamo wanasiasa wilayani hapa na mkoani Mara, waliochukizwa na uamuzi wake wa kuagiza wakwepa kodi kudhibitiwa ikiwamo kutiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani.

“Katika hili la mapato ya Serikali simuogopi mtu yeyote zaidi ya Mungu anayenipa pumzi na Rais Magufuli aliyeniteua,” alisema Luoga.

Naye ofisa maendeleo wa Halmashauri ya Mji Tarime, Emmanuel Sizo alisema wanawake ni warejeshaji wazuri wa mikopo ikilinganishwa na vijana ambao baadhi yao wanatokomea baada ya kupokea fedha. Sizo alisema hadi sasa halmashauri inavidai vikundi vya vijana zaidi ya 10 milioni.