Walia kupoteza wenza na watoto wao

Waombolezaji wakiweka mashada ya maua kwenye kaburi la ndugu yao wakati wa mazishi yaliyofanyika katika eneo la Bwisya jana. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Zipo familia zilizopoteza idadi kubwa ya watu na kuacha pengo na simanzi litakalochukua muda mrefu kuliziba.

Ukerewe. Mitaa ya Kijiji cha Bwisya katika Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe imejaa vilio kutokana na familia nyingi kupoteza ndugu na jamaa katika ajali hiyo.

Zipo familia zilizopoteza idadi kubwa ya watu na kuacha pengo na simanzi litakalochukua muda mrefu kuliziba.

Mzee Mtoroki Masena (75), aliyempoteza mwanae Nyanjira (43), alisema ajali hiyo imemwondolea pia mkewe Buhinda (64) waliyedumu naye kwa miaka 45 tangu walipooana mwaka 1973.

Mzee Masena aliiomba Serikali kununua kivuko kipya chenye uwezo wa kusafirisha abiria wengi na mizigo kati ya kisiwa cha Ukara na kisiwa kikuu cha Ukerewe.

Theodora Maira (46), ambaye katika ajali hiyo alimpoteza mumewe, January Bwenge (52) na mtoto wake, Paschal (7) alisema aliiomba Serikali kuchukua hatua kudhibiti ajali zinazoteketeza maisha ya watu wasio na hatia.

“Mume na mtoto wangu walivuka maji kwenda kwenye gulio la Bugolora linalofanyika kila Alhamisi kwa ajili ya kununua mahitaji ya shule. Ningejua yatatokea haya ningwazuia kwenda,” alisema na kuongeza kuwa Paschal alikuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Bwisya.

Jana, barabara inayotoka Kituo cha Afya Bwisya kwenda ghati ya Bwisya ilikuwa na watu wengi waliokwenda kuchukua miili ya ndugu zao.

Changamoto za ugeni mkubwa

Kijiji hicho kilipata ugeni mkubwa pengine kuliko muda wowote katika historia yake.

Ugeni huo uliokana na wingi wa watu waliofika kutambua na kuchukua miili ya ndugu zao waliokufa baada ya kivuko cha Mv Nyerere kuzama mchana wa Alhamisi.

Kilijaa wageni wa kila aina kuanzia viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi na mashirika ya umma, waandishi wa habari na makundi mbalimbali ya wananchi.

Kama wahenga walivyosema kwamba majanga hayana hodi, ugeni huo uliibua changamoto mbalimbali ikiwamo sehemu ya kulala na upatikanaji wa huduma nyingine muhimu.

Kutokana na hali hiyo, meli ya Serikali ya Mv Clarias iligeuka makazi kwa baadhi ya wageni hao wakiwamo waandishi wa habari ambao licha ya kulala kwenye viti, waliitumia kama kituo cha habari, wakijachi simu zao na vifaa vingine vya kazi.

“Mimi hata sikubahatika kupata kiti cha kukalia. Nimelala sakafuni kwenye sehemu ya kupakia mizigo ndani ya meli,” alisema Sarah Onesmo mwandishi wa habari wa Clouds Media.

Wingi huo ulikuwa fursa kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa katika maduka ya rejereja. Blanketi na mashuka ya kujifunika ni kati ya bidhaa zilizokuwa adimu katika Ukara, Blanketi ndogo lililokuwa likiuzwa kwa Sh7,000 hadi Sh8,000 liliuzwa hadi Sh15,000.

Mashuka maarufu ya Kimasai pia yaliuzwa Sh15,000 badala ya Sh10, 000 ya awali.

“Nimeuza blanketi na mashuka yote kwa bei karibia mara mbili ya bei ya awali. Wewe ndio unamalizia hili blanketi moja iliyosalia,” alisema Neema Joseph akiwa dukani kwake.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akiuza blanketi kwa mmoja wa waandishi wa Mwananchi alisema alilazimika kupandisha bei kutokana na mahitaji kuwa makubwa kulinganisha na bidhaa alizokuwa nazo dukani.