Madeni yawatesa walimu tisa

Muktasari:

Walikopa sasa wameshindwa kulipa

Mbogwe. Walimu tisa wa shule za msingi Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wanadaiwa kukacha kufika kazini kukwepa madeni waliyokopa kutoka taasisi mbalimbali za fedha na watu binafsi.

Hii inatokana na hofu ya kukamatwa na wadeni wao ambao tayari wamekamilisha taratibu za kisheria kuwezesha kuwatia mbaroni na kupiga mnada dhamana zao kama njia ya kuwashinikiza wakamilishe marejesho.

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT), Wilaya ya Mbogwe, Victor Tandise ameliambia Mwananchi jana Alhamisi kuwa ofisi yake tayari imefanya vikao kadhaa na uongozi wa taasisi zinazowadai walimu hao kuangalia namna bora ya kumaliza madeni hayo.

Mkurugenzi wa taasisi ya Salivan and Son’s Financial Services ambayo ni miongoni mwa taasisi zinazowadai walimu hao, Salvan Kabati alisema kampuni yake imefikia uamuzi wa kutafuta ufumbuzi wa kisheria kurejesha fedha zake baada ya walimu hao kukiuka mikataba ya mikopo yao.

“Taasisi yangu iliwakopesha walimu 47 wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe; 38 wamekamilisha marejesho ya mikopo yao lakini hawa tisa waliosalia tunawadai zaidi ya Sh24 milioni na wamekiuka mikataba na kubadilisha mfumo wa benki uliokuwa ukitumika kwenye marejesho,” alisema Kabati.

Akizungumzia kuwasaka walimu hao, kabati alisema taasisi yake imefikia hatua hiyo baada ya wahusika kutoonyesha nia ya kulipa deni licha ya kupewa muda wa ziada.