Waliofariki dunia ajali ya MV Nyerere wafikia 209

Muktasari:

  • Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema miili 172 imetambuliwa na 112 imechukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazik

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere imefikia 209.

Wakati Kamwelwe akieleza hayo leo jioni Jumamosi Septemba 22, 2018, mkuu wa Mkoa wa Mwanza  John Mongella amesema meli ya MV Nyehunge kutoka Mwanza inaelekea kisiwa cha Ukara ikiwa na vifaa maalum vitakavyotumika kukinyanyua kivuko hicho ili kurahisisha uokoaji na taratibu nyingine.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, Kamwelwe amesema watu waliopatikana wakiwa hai ni 41, baada ya mmoja kuongezeka leo ambaye ni mhandisi wa kivuko hicho, Alphonce Charahani.

Waziri Isack Kamwelwe amesema miili iliyotambuliwa ni 172, kati ya hiyo 112  tayari imeshachukuliwa na ndugu kwa ajili ya maziko.

“Miili 37 bado haijatambuliwa, nieleze tu kuwa ndugu wanaochukua miili kwa ajili ya maziko wanapatiwa ubani wa Sh500,000 kama ambavyo Serikali imeahidi,” amesema Kamwelwe.