Waliofariki dunia ajali ya kivuko wafikia 218

Muktasari:

  • Miili ya watu 171  iliyoopolewa katika zoezi la uokoaji kwenye ajali ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere imetambuliwa

Ukerewe. Miili 171 kati ya 218 iliyoopolewa baada ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere juzi Septemba 20, 2018 imetambuliwa na ndugu.

Ndugu, jamaa na wananchi wamepiga kambi eneo la bandari ya Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe tangu kazi ya uokoaji ilipoanza.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) leo Jumamosi Septemba 22, 2018 saa  2 usiku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema wapo baadhi ya ndugu wanaotaka kuwazika wapendwa wao kisiwani humo.

Amesema kwa sasa taratibu mbalimbali zinafanyika, ikiwa ni pamoja na jitihada za kukinyanyua kivuko hicho  kazi ambayo itafanywa na timu ya waokoaji.

“Kesho kuanzia saa 2 asubuhi kamati itafanya maziko ya miili 47,” amesema Mongella.

Miili iliyoopolewa imehifadhiwa katika Kituo cha afya cha Bwisya.