VIDEO: Waliofariki dunia kuzama kwa kivuko wafikia 86

Muktasari:

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella hadi leo saa 4 asubuhi Septemba 21, 2018 jumla ya maiti 86 zimeopolewa

Mwanza. Saa zaidi ya 20 tangu kuzama kivuko cha MV Nyerere, idadi ya watu waliokufa imefikia 86.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella hadi leo saa 4 asubuhi Septemba 21, 2018 jumla ya maiti 86 zimeopolewa .

Akihojiwa na  Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Mongella amesema miili 42 imepatikana leo asubuhi, wakati mingine 44 ilipatikana jana.

“Watu 40 wameokolewa wakiwa hai, bado tunaendelea na zoezi la uokoaji,” amesema Mongella.

MCL Digital  ipo eneo kilipozama kivuko hicho imeshuhudia zoezi la uokoaji likiendelea na kuongozwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliani, Isack Kamwelwe, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali  Simon Sirro

Katika zoezi hilo la uokoaji, Mongella amekuwa akitoa maelekzo ya mahali pa kuhifadhia miili, ambayo inapelekwa katika kituo cha afya cha Bwisya kilichopo umbali wa mita takribani 300 kutoka kilipozama kivuko hicho.

“Tupo ndani ya boti hapa na uokoaji unaendelea. Kuna boti saba zimekizunguka kivuko kilichozama ambacho kinaonekana kidogo sehemu yake ya chini,” amesema mwandishi Wetu.

Kivuko hicho kilizama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga kisiwa cha Ukara.

Kilikuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kinadaiwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100, wengi wakiwa wanaelekea kwenye gulio.