Waliohusika na uendeshaji, usimamizi wa kivuko kilichozama wakamatwe

Muktasari:

Serikali imetoa kauli hiyo leo kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi  ambapo pia imetangaza siku nne za maombolezo kuanzia leo, bendera kupepea nusu mlingoti

Dodoma. Siku moja baada Kivuko cha Mv Nyerere kuzama, Serikali imeagiza wahusika wote kwenye uendeshaji na usimamizi wa kivuko hicho na viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kukamatwa na kuhojiwa ili kubaini ushiriki wao.

Rais John Magufuli ameagiza bendera ya Taifa kupepea nusu mlingoti kwa siku nne kuanzia leo Septemba 21, 2018 ikiwa ni hatua ya kuomboleza vifo vilivyotokana na ajali hiyo.

Akizungumza leo jijini hapa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amesema hadi kufikia leo saa 1:10 usiku, miili ya watu 127 ilikuwa imeopolewa huku 40 wakiokolewa wakiwa hai.

"Mara baada ya kutokea ajali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wananchi inaendelea na shughuli za uokoaji na utafutaji wa miili bado unaendelea," amesema

Balozi Kijazi amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni kivuko hicho kubeba abiria wengi kuliko uwezo wake.

Amesema kivuko hicho kinatakiwa kubeba abiria 101 na kwamba tayari uchunguzi wa kina kubaini sababu nyingine umeanza.

Amesema baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo wa kina taarifa kamili itatolewa kwa wananchi.

"Mambo mengine yanazuilika, naamini kama viongozi wangechukua hatua mapema  janga hili lingeweza kuzuilika.”

“Kila mahali panapohusisha maisha ya binaadamu, tuwe makini, tuwe macho maisha ya Watanzania yasihatarishwe kwa  uzembe," amesema Balozi Kijazi

Hata hivyo, leo MCL Digital imezungumza na mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Johansen Kahatano amesema kwa sasa udhibiti wa vyombo vya majini haupo katika mamlaka hiyo bali unafanywa na Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Tasac).