Waliokutwa na nyuki kwenye kiroba waendelea kusota rumande

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei

Muktasari:

  • Watu hao walikamatwa Septemba 16 wakienda kituo cha majumuisho ya kura ya udiwani wa Nkuyu jijini Mbeya

Mbeya. Watu wanne wanaoshikiliwa na polisi wilayani Kyela jijini Mbeya kwa tuhuma za kukutwa na bastola, cheni ya kuchezea karate, mfuko uliojazwa nyuki, 'radio call' na simu  tano za mkononi wanaendelea kusota mahabusu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema watu hao walikamatwa Jumapili wiki iliyopita wakijiandaa kwenda kufanya vurugu kwenye chumba cha kujumlishia kura za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Nkuyu wilyani Kyela.

Matei amesema leo ofisini kwake kwamba, watu hao baada ya kukamatwa na kufikishwa kituo kikuu cha polisi Kyela waligoma kuandika maelezo kwa madai hadi wawepo mawakili wao.

''Siku ile walipokamatwa walitakiwa kuandika maelezo lakini walidai hawawezi kufanya hivyo bila ya kuwepo kwa mawakili wao.”

“Hivyo jana ndiyo mawakili wao walikwenda na wakahojiwa mbele ya mtetezi wao na muda wowote watafikishwa mahakamani na mpaka sasa wapo ndani hawakupata dhamana," amesema.

Kamanda Matei amesema  waliwakamata watu hao baada ya kupata taarifa za kiintelijensia kuwa wamekodiwa na chama kimoja cha upinzani kwa ajili ya kufanya vurugu kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani kata hiyo.

“Watu hao walikamatwa wakiwa ndani ya gari aina ya Nissan Pick Up na baada ya kupekuliwa walikutwa wakiwa na silaha na vifaa mbalimbali ambavyo ni bastola moja aina ya Browing yenye namba A.82712, risasi 37 na magazine mbili, kifurushi kimoja ambacho ndani yake kilifungiwa wadudu aina ya nyuki,” amesema

Amesema vitu vingine ni cheni moja ya kuchezea karate, Radio call mbili, Mzula mmoja (Kofia ya Kininja), simu tano za mkononi aina ya Itel – 3 na Tecno 2.

Amesema  watu hao walikamatwa wakati wakiekelea kituo cha majumuisho ya kura za udiwani kata hiyo na walipoulizwa wanakwenda wapi walijibu 'tunakwenda kulinda kura'.