Waliokwama mgodini waokolewa hai

Muktasari:

*"Kila mtu yuko nje," alisema James Wellsted, msemaji wa kampuni ya Sibanye-Stillwater inayomiliki mgodi huo. “Kuna watu kadhaa waliokumbwa na tatizo la kuishiwa maji mwilini na shinikizo la damu lakini hakuna madhara".

*Mgodi wa Beatrix ulioko katika mji wa Welkom, karibu kilomita 290 (maili 180) kusini-magharibi mwa Johannesburg unamilikiwa na kampuni ya madini ya Sibanye-Stillwater.

*Ajali hiyo inadhaniwa kwamba ilitokea baada ya dhoruba kupiga nguzo ya umeme karibu na eneo la mgodi na kusababisha nishati hiyo kukatika. Mgodi uko mita 1000 sawa na futi 3,280 chini ya ardhi.

Johannesburg, Afrika Kusini. Wafanyakazi wote 955 waliokuwa wamekwama chini ya mgodi wa Beatrix wameokolewa na kutoka salama mapema leo.

Wafanyakazi hao walikuwa wamenaswa chini ya ardhi tangu ulipokatika umeme Jumatano usiku.

"Kila mtu yuko nje," alisema James Wellsted, msemaji wa kampuni ya Sibanye-Stillwater inayomiliki mgodi huo. “Kuna watu kadhaa waliokumbwa na tatizo la kuishiwa maji mwilini na shinikizo la damu lakini hakuna madhara".

Afrika Kusini ni mzalishaji mkubwa wa madini ya dhahabu lakini usalama katika sekta hiyo mara nyingi huacha maswali.

Mgodi wa Beatrix ulioko katika mji wa Welkom, karibu kilomita 290 (maili 180) kusini-magharibi mwa Johannesburg unamilikiwa na kampuni ya madini ya Sibanye-Stillwater.

Ajali hiyo inadhaniwa kwamba ilitokea baada ya dhoruba kupiga nguzo ya umeme karibu na eneo la mgodi na kusababisha nishati hiyo kukatika. Mgodi uko mita 1000 sawa na futi 3,280 chini ya ardhi.

Lakini Ijumaa asubuhi hatimaye umeme ulirejeshwa na kuwezesha wafanyakazi kutolewa.

"Ilikuwa na shida, hakukuwa na hewa ya kutosha," alisema mfanyakazi mmoja Mike Khonto. "Shukrani menejimenti yetu ilifanikiwa kutuletea chakula na maji."

Baada ya kuokolewa walipewa chakula na maji ya kuoga kabla ya kufanyiwa uchunguzi na kupewa matibabu.

Wellsted alisema "hakuna dalili hadi sasa kwamba hakuna mtu yeyote aliyekuwa katika dhiki" lakini ulikuwa "uzoefu wa kutisha".

Vifo zaidi ya 80 vilirekodiwa kutokea katika migodi ya Afrika Kusini mwaka 2017.