Waliopewa msaada wa mabati watakiwa kukamilisha ujenzi haraka

Muktasari:

Kiomoni alitoa ushauri huo juzi wakati Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula alipokuwa akikabidhi mabati 700 yenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni kwa kaya za kata nne jijini Mwanza ambazo ziliezuliwa paa baada ya mvua iliyoambatana na upepo kunyesha Februari 2.

Mwanza. Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amewataka wakazi wa kata nne waliopokea msaada wa mabati 700 baada ya nyumba zao kuezuliwa na mvua, kujenga haraka ili kuepuka usumbufu wa kuendelea kuhifadhiwa na ndugu na majirani.

Kiomoni alitoa ushauri huo juzi wakati Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula alipokuwa akikabidhi mabati 700 yenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni kwa kaya za kata nne jijini Mwanza ambazo ziliezuliwa paa baada ya mvua iliyoambatana na upepo kunyesha Februari 2.

“Msaada huu ni sehemu ya ahadi niliyotoa baada ya kupigiwa simu nikiwa bungeni kwamba baadhi ya wakazi wa jimbo langu hawana makazi, kutokana na nyumba zao kuezuliwa na nyingine kuanguka kutokana na mvua iliyokuwa imeambatana na upepo mkali,” alisema Mabula.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwanza Huduma Limited iliyonunua vifaa hivyo, Zully Nanji alisema ni matarajio yake kuwa mabati hayo ambayo ni sehemu ya faida ya biashara yake yatawafikia walengwa na kutumika kwa ujenzi wa nyumba.