Wanachama 13 Chadema wafikishwa mahakamani

Muktasari:

Washtakiwa kwa makosa mawili, warejeshwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana

Tunduma. Wanachama 13 wa Chadema leo, Jumatatu Julai 16, 2018, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe kujibu mashtaka mawili ya shambulio la kudhuru mwili na kuzuia polisi kutekeleza wajibu wao.

Washtakiwa hao ni Elia Mwaluswaswa, Rafael Jarson, Rehema Isaya, Gabriel Kampuni, Huruma Tenson, Tunae Paul, Steven Evarist, Asha Maxson, Naomi Lucas na Sety Saul.

Wengine ambao ni madiwani ni Emmanuel  Mwalukasa (Mpande), Jailo Maheya (Katete) na Rebeca Adam (viti maalumu).

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Zabibu Mpangule, Mwendesha Mashtaka Joel Mori amedai  mshtakiwa wa kwanza na wa pili (Mwaluswaswa na Jarson), wanashtakiwa kwa kufanya shambulio la kudhuru mwili na kumzuia askari kutekeleza jukumu la kuwakamata.

Amesema kosa la pili linawahusu washtakiwa wote 13, kubainisha kuwa Julai 14 katika eneo la Mwaka-Tunduma walimzuia askari Gawile kumkamata Herode Jivava na Isakwisa Thobias.

Washtakiwa hao wamekana mashtaka hayo na Mori ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine.

 

Wakili wa upande wa utetezi, Boniface Mwabukusi ameiomba Mahakama kuwapatia dhamana yenye masharti nafuu.

 

“Kwa kuzingatia aina ya mashtaka yana dhamana na upande wa Jamhuri umesema upelelezi haujakamilika, hivyo naomba Mahakama yako tukufu iwape dhamana  yenye masharti nafuu," amesema Mwabukusi.

 

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mpangule alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini watatu wenye mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh20 milioni na barua ya ofisa mtendaji wa kata.

 

Licha ya Mwabukusi kuwasilisha ombi jingine, akitaka washtakiwa hao kuruhusiwa kuwa na wadhamini wawili pamoja na kupokea barua walizokuwa nazo, hakimu huyo alikataa ombi hilo.

 

“Nani kawaeleza mje na wadhamini wawili? Ina maana huko nje kuna Mahakama nyingine inayopanga kufanya hivyo. Sasa nasema wadhamini ni watatu na barua za watendaji kata,”amesema Hakimu Mpangule.

“Tofauti na hapo hata kesho mtakuja kutimiza masharti hayo na si vinginevyo. Pia wakili Mwabukusi unaweza kukataa rufaa kwa uamuzi huu.”

Keshi hiyo imeahirishwa hadi Julai 26, 2018 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Nje ya mahakama, Mwabukusi aliwataka wafuasi wa chama hicho kuwa watulivu wakati akiendelea na taratibu za kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.