VIDEO-Wanafunzi, ACT Wazalendo wamtaka Mwigulu ajiuzulu

Muktasari:

  • TSNP imetoa kauli hiyo leo Februari 18, 2018 ikiwa ni siku moja tangu kupigwa risasi kwa  mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline aliyekuwa katika daladala wakati polisi walipowatawanya wafuasi wa Chadema.

Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) na Chama cha ACT-Wazalendo wamemwomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Mwigulu Nchemba kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji kwa maelezo kuwa ameshindwa kusimamia amani.

TSNP imetoa kauli hiyo leo Februari 18, 2018 ikiwa ni siku moja tangu kupigwa risasi kwa  mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline aliyekuwa katika daladala wakati polisi walipowatawanya wafuasi wa Chadema.

Kauli ya mtandao huo na chama hicho imetolewa leo baada ya viongozi wao kuzungumza na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa TSNP Taifa, Abdul Nondo amesema iwapo Mwigulu hatajiuzulu wadhifa wake, wamemuomba Rais John Magufuli kutengua uteuzi wake.

“Kwa kuwa hivi sasa matukio haya yamekuwa yakishamiri na kushika kasi; watu kutekwa, kupotea, kupigwa risasi na kuuwawa ni muda muafaka sasa kwa Mwigulu kuchukua uamuzi wa kujiondoa katika wizara kuonyesha uwajibikaji,” amesema.

Amebainisha kuwa mwaka 1977 Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Ali  Hassan Mwinyi wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alijiuzulu baada ya polisi  kutumia nguvu dhidi ya raia.

"Tunaamini kwamba huo utakuwa ni mwanzo wa kukaribisha mabadiliko katika Jeshi la Polisi kwani kuondoka kwa mkuu kutawafanya walio chini yake kuondolewa,” amesema.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Idara ya Sheria TSNP,  Deogratias Mahinyila amesema taasisi yao kupitia wanasheria wao na wanasheria mbalimbali watawasaidia walezi na wazazi wa mwanafunzi huyo kufungua kesi ya madai mahakamani, kutokana na uzembe uliofanywa na polisi ili iwe fundisho.

"Tunataka hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya askari polisi waliotenda unyama huu na kukatisha haki ya kusoma na kuishi kwa mwanafunzi mwenzetu kwani wamekiuka sheria na maadili ya kazi yao, katika kulinda amani ya raia," amesema.

Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba awajibike kwa kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu ameshindwa kukomesha mfululizo wa mauaji ya watu wasio na hatia.

 

Pia, wamewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa nao wajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ikiwamo kulinda usalama wa raia na mali zao.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Licapo Bakari amesema matukio mengi ya mauaji na kupotea kwa watu yanatokea na viongozi hao hawachukui hatua zozote kukomesha hali hiyo.

Amesisitiza kwamba wote wanaouawa na kutoweka katika mazingira tatanishi ni vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa na chachu ya mabadiliko ambayo inatakiwa kulindwa kwa mustakabali wa nchi hii.

Bakari amesema vijana wa ACT Wazalendo wanalaani mauaji ya Akwilina, kwamba tukio la kuuawa kwa binti huyo siyo la kwanza, siku chache zilizopita kiongozi wa Chadema kata ya Hananasifu, Daniel John naye aliuawa na mwili wake kuokotwa kwenye fukwe za Coco.

"Tunataka uchunguzi huru ufanyike kwa kuchunguza matukio yote kuanzia hili la mwanafunzi wa NIT na mengine yote ya mauaji na utekaji," amesema.

Wakati huohuo, Bakari amewataka viongozi wote wa vyama vya siasa kukutana na kupanga mikakati na siku ambayo wanajumuika pamoja na wananchi kupaza sauti na kusema matukio hayo sasa basi.

"Wote tunaipenda nchi yetu, hatupendi kuona ikipotea. Viongozi wa dini, vijana, wanafunzi na wananchi wote tuungane pamoja kupinga ukatili unaotokea ndani ya nchi yetu wenyewe," amesema.

Imeandikwa na Peter Elias, Herieth Makwetta na Allende Juma